Warner Music na 'Udio' Waweka Silaha Chini, Waungana Kutengeneza Pesa kwa AI

it | Fri Nov 21 2025


Warner Music na 'Udio' Waweka Silaha Chini, Waungana Kutengeneza Pesa kwa AI

Kuna msemo wa wahenga usemao, "Ukiona huwezi kushindana nao, ungana nao." Huu ndio mkakati mpya ambao makampuni makubwa ya muziki duniani yameanza kuutumia dhidi ya wimbi la Akili Mnemba (AI). Baada ya miezi kadhaa ya kutishiana kuburuzana mahakamani kwa madai ya wizi wa hakimiliki, kampuni kubwa ya muziki ya Warner Music Group (inayosimamia mastaa kama Ed Sheeran na Cardi B) imetangaza 'suluhu ya kibiashara' na kampuni ya AI ya Udio.


Katika makubaliano yaliyotangazwa tarehe 19 Novemba, pande hizi mbili zimekubaliana kufuta kesi zote zilizokuwepo na badala yake kushirikiana kuanzisha jukwaa jipya la kutengeneza muziki kwa kutumia AI ifikapo mwaka 2026.


Biashara Mpya: Kulipa ili Kutengeneza 'Hit'


Makubaliano haya yanafungua ukurasa mpya katika historia ya muziki. Jukwaa hilo litakalozinduliwa litawaruhusu watumiaji kutengeneza nyimbo mpya kwa kutumia AI, lakini kwa njia halali. Tofauti na zamani ambapo AI ilikuwa "inaiba" sauti na midundo ya wasanii bila ruhusa, mfumo huu mpya utatumia nyimbo ambazo zimelipiwa leseni.


Hii ina maana gani? Mtumiaji atalipa ada ya mwezi (subscription), na pesa hizo zitagawanywa kama mirabaha (royalties) kwa wasanii na watunzi wa nyimbo ambazo AI imetumia kujifunza au kutengeneza muziki huo. Ni mfumo wa "kula na kuliwa" unaolenga kutoa faida kwa pande zote—teknolojia inapata data, na msanii anapata pesa.


Hatua hii ya Warner inafuata nyayo za mpinzani wao, Universal Music Group (UMG), ambao mwezi uliopita walifanya makubaliano kama hayo na Udio. Hii inaashiria kuwa vita ya hakimiliki kati ya binadamu na roboti katika muziki inageuka kuwa ubia wa kibiashara.


Suno Nayo Yapata 'Jeuri ya Pesa'


Wakati Warner na Udio wakigonga glasi, kampuni nyingine kubwa ya AI ya muziki, Suno, nayo imetangaza habari njema. Suno imefanikiwa kukusanya mtaji mpya wa Dola za Kimarekani milioni 250 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 660).


Uwekezaji huu, ambao umehusisha vigogo wa teknolojia kama Nvidia, unaifanya Suno sasa kuwa na thamani ya soko ya Dola bilioni 2.45 (takriban TZS Trilioni 6.5). Hii ni pesa ndefu sana, inayoonyesha kuwa wawekezaji wana imani kubwa kuwa mustakabali wa muziki upo mikononi mwa AI. Inasemekana Suno nayo iko mbioni kuingia mikataba na lebo kubwa za muziki ili kuhalalisha biashara yake.


Hofu ya Kupotea kwa 'Uhalisia'


Licha ya pesa hizi na makubaliano, kuna hofu inayoendelea kutanda. Je, mashabiki wataweza kutofautisha kati ya wimbo uliopigwa na prodyuza binadamu (kama S2kizzy au Abbah) na ule uliotengenezwa na kompyuta?


Utafiti mpya kutoka mtandao wa kusikiliza muziki wa Deezer wa Ufaransa umetoa majibu ya kutisha: Asilimia 97% ya wasikilizaji wameshindwa kutofautisha kati ya muziki wa AI na ule wa binadamu! Hii ina maana kuwa AI imefikia kiwango cha juu sana cha ubora kiasi kwamba sikio la kawaida halitoi tofauti.


Hali hii inazua mjadala mpya: Ikiwa roboti inaweza kutengeneza wimbo mtamu kuliko binadamu kwa sekunde chache, nini kitatokea kwa vipaji vyetu? Wakati Wamarekani (kulingana na utafiti wa Luminate) wakionekana kukubali AI isaidie kwenye video (VFX), bado wana wasiwasi na AI kuandika mashairi au kuigiza kama binadamu.


Kwa tasnia ya muziki ya Tanzania (Bongo Flava), huu ni wakati wa kukaa chonjo. Mabadiliko haya ya teknolojia yanakuja kwa kasi, na mfumo wa kulinda hakimiliki na kukusanya mirabaha utalazimika kubadilika ili kuendana na zama hizi mpya ambapo "msanii" anaweza kuwa programu ya kompyuta.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.