Katika kile kinachoweza kutajwa kama "Suluhu ya Mwaka" kwenye tasnia ya burudani duniani, vita kali ya kisheria iliyokuwa ikifukuta kati ya kampuni gwiji ya muziki duniani, Warner Music Group (WMG), na wababe wa teknolojia ya muziki wa Akili Mnemba (AI), Suno, imefikia tamati kwa kishindo. Badala ya kuendelea kuvutana mahakamani, pande hizi mbili zimeamua kuweka silaha chini na kuingia ubia wa kibiashara, hatua inayotazamiwa kubadili kabisa uelekeo wa soko la muziki duniani.
Tukio hili linafanana na msemo wa wahenga, "Hasira hasara, biashara maelewano." Warner Music, ambayo inasimamia kazi za mastaa wakubwa duniani, ilikuwa imewaburuza Suno mahakamani (pamoja na kampuni nyingine ya Udio) ikidai kuwa kampuni hizo ziliiba nyimbo zao na kuzitumia kufundishia mifumo yao ya AI bila idhini wala malipo. Lakini sasa, upepo umebadilika.
Kutoka Mahakamani hadi Studio
Tarehe 25 (saa za Marekani), Warner Music Group ilitangaza rasmi kuwa imefuta kesi hiyo na kuingia mkataba wa ushirikiano na Suno. Hii inafuatia nyayo za washindani wao, Universal Music Group (UMG), ambao pia walimaliza tofauti zao na kampuni ya Udio kwa mtindo huohuo hivi karibuni.
Robert Kyncl, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa WMG, ameielezea hatua hii kama "makubaliano ya kihistoria" yenye faida kwa jumuiya nzima ya wasanii. "Suno inakua kwa kasi sana kwa watumiaji na mapato. Ushirikiano huu unatupa fursa mpya ya kutengeneza mifumo ya mapato na kuongeza uzoefu wa mashabiki wa muziki," alisema Kyncl.
Kwa lugha nyepesi, mabosi wa muziki wamegundua kuwa huwezi kushindana na teknolojia, ni bora kuungana nayo ili "kupiga mkwanja" pamoja.
Mfumo Mpya: "Hakuna cha Bure"
Kuanzia mwakani, mambo yatabadilika. Suno inatarajiwa kuzindua mfumo mpya wenye leseni maalum. Katika mfumo huu, kama mtumiaji atataka kutengeneza wimbo kupitia AI ya Suno na kuupakia kwenye mitandao ya kusikiliza muziki (kama Spotify, Boomplay au Apple Music), itabidi awe na usajili wa kulipia (Paid Subscription).
Hii ni mbinu ya kibiashara inayohakikisha kuwa wakati watu wanafurahia kurahisishiwa kazi na AI, wenye hakimiliki (wasanii na lebo) nao wanapata 'keki' yao. Pia, idadi ya nyimbo zitakazoweza kupakuliwa (download) kwa mwezi itadhibitiwa kulingana na kifurushi cha mtumiaji.
Wasanii Kupewa Machaguo
Kipengele kingine cha kuvutia katika makubaliano haya ni uhuru wa wasanii. Wasanii walio chini ya Warner Music watapewa nafasi ya kuridhia au kukataa sauti zao, picha, au mitindo yao ya utunzi kutumiwa na watumiaji wa Suno.
Fikiria kama msanii kama Diamond Platnumz au Harmonize (kama wangekuwa chini ya WMG) angeruhusu sauti yake itumike, basi shabiki angeweza kuingia Suno na kuamuru: "Nitungie wimbo wa mapenzi kwa sauti ya Diamond," na AI ingefanya kazi hiyo kwa sekunde, huku msanii akilipwa. Hii ndiyo teknolojia ambayo Mikey Shulman, Mkurugenzi wa Suno, anasema "itafafanua upya thamani ya muziki."
Historia Yajirudia: Kutoka MP3 hadi AI
Wadadisi wa mambo wanasema hatua hii ya lebo kubwa za muziki (Warner na Universal) kukumbatia AI inafanana na ilivyotokea miaka ya 2000 mwanzoni. Wakati huo, teknolojia ya MP3 ilipoingia na watu kuanza kupakua nyimbo bure kwenye mtandao (kumbuka enzi za kuchoma CD), lebo zilianza kwa kupambana na mitandao kama Napster mahakamani.
Lakini mwishowe, waligundua kuwa hawawezi kuzuia maji kwa mikono. Suluhisho likawa kuanzisha mifumo ya 'Streaming' (kama Spotify na Apple Music) ambayo iligeuza maharamia kuwa wateja wa kulipia. Sasa hivi, historia inajirudia kwenye AI; badala ya kupigana nayo, wameamua kutengeneza mfumo wa kulipana kihalali.
Kwa sasa, kati ya 'Wababe Watatu' wa muziki duniani (The Big Three), ni Sony Music pekee ambayo bado haijatangaza rasmi kumaliza bifu lake na Suno au Udio, ingawa tetesi zinasema nao wako njiani kufuata mkumbo huo. Kampuni mpya ya 'Klay' tayari imeshamalizana na wakubwa wote watatu.
Hili ni funzo kubwa kwa tasnia ya muziki nchini Tanzania (Bongo Flava). Wakati teknolojia inabadilika, ni muhimu kwa wadau wetu, COSOTA, na wasanii kuanza kufikiria jinsi ya kutengeneza pesa kupitia AI badala ya kuogopa kuwa itawapokonya ajira.