Uamuzi wa Kihistoria Marekani: Google na Kampuni ya AI Kuwajibika kwa Kifo cha Kijana Aliyeongea na Chatbot

it | Sat Jun 28 2025


Uamuzi wa Kihistoria Marekani: Google na Kampuni ya AI Kuwajibika kwa Kifo cha Kijana Aliyeongea na Chatbot

Katika uamuzi unaoweza kubadilisha jinsi kampuni za teknolojia zinavyowajibika kisheria, mahakama ya shirikisho nchini Marekani imetoa uamuzi kwamba kampuni kubwa ya teknolojia, Google, na kampuni chipukizi ya Akili Mnemba (AI), Character.AI, lazima zijibu mashtaka kuhusiana na kifo cha kijana wa miaka 14 aliyejiua baada ya kuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na roboti la mazungumzo (chatbot).


Tukio hili la kuhuzunisha linamhusu kijana Sewell Setzer kutoka Florida, ambaye alikutwa amejinyonga. Uchunguzi ulionyesha kuwa kwa takriban mwaka mmoja, kijana huyo alikuwa akitumia muda mwingi kwenye mazungumzo na chatbot kutoka jukwaa la Character.AI. Jukwaa hili, lililoundwa na wahandisi wa zamani wa Google, linawaruhusu watumiaji kuunda na kuzungumza na wahusika wa AI ambao huiga watu halisi au wahusika kutoka kwenye filamu na vitabu. Setzer alikuwa akizungumza na AI iliyoiga mhusika ‘Daenerys Targaryen’ kutoka tamthilia maarufu ya ‘Game of Thrones’.


Inaripotiwa kuwa kijana huyo alikuwa akimweleza chatbot huyo hisia zake, akisema maneno kama "nina huzuni sana" na "nataka kufa." Ujumbe wake wa mwisho kwa chatbot huyo ulikuwa "nakuja kwako sasa hivi," kabla ya kuchukua uhai wake.


Mama yake mzazi, Megan Garcia, ndiye aliyepeleka kesi hii mahakamani, akidai kuwa mazungumzo na chatbot huyo yalichochea na kuzidisha sonona (depression) ya mwanae na hatimaye kumsukuma kujiua. Alisema kuwa kutokana na mazungumzo hayo, mwanae alipoteza hamu ya masomo na kujitenga na jamii.


Kwa upande wao, Google na Character.AI ziliiomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo. Hoja yao kuu ilikuwa kwamba maneno yanayotolewa na chatbot yanalindwa na katiba chini ya "uhuru wa kujieleza." Google pia ilijaribu kujitenga na lawama, ikidai kuwa ni kampuni tofauti kabisa na Character.AI.


Hata hivyo, Jaji Anne Conway alikataa hoja zote za kampuni hizo. Katika uamuzi wake, alisema kuwa maneno yanayotengenezwa na Mfumo Mkubwa wa Lugha (LLM) wa AI hayastahili kupata ulinzi wa kikatiba wa "uhuru wa kujieleza" katika muktadha huu. Vilevile, alikataa hoja ya Google ya kutaka kujiondoa kwenye kesi hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa waanzilishi wa Character.AI walirejea kufanya kazi Google na kampuni hizo zina mkataba wa kipekee wa huduma.


Wakili wa familia, Mitali Jain, aliuita uamuzi huu "wa kihistoria," akisema unaweka "msingi mpya wa kisheria kuhusu uwajibikaji katika sekta nzima ya Akili Mnemba na teknolojia kwa ujumla." Kesi hii sasa inaonekana kama kipimo muhimu kitakachoweka mipaka ya uwajibikaji wa kampuni za AI kwa madhara yanayoweza kusababishwa na bidhaa zao.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.