Soko Jipya la Ajabu: Sauti za Mastaa Waliokufa na Walio Hai Sasa Zinauzwa Kihalali

it | Thu Nov 13 2025


Soko Jipya la Ajabu: Sauti za Mastaa Waliokufa na Walio Hai Sasa Zinauzwa Kihalali

Kampuni ya teknolojia ya Akili Mnemba (AI) ya ElevenLabs imeleta mapinduzi mapya ambayo huenda yakabadilisha kabisa tasnia ya matangazo na burudani duniani. Wamezindua rasmi soko jipya la kidijitali liitwalo 'Iconic Voices' (Sauti za Kipekee), ambalo linatoa fursa kwa makampuni na watengenezaji wa maudhui kununua na kutumia sauti za watu maarufu duniani zilizotengenezwa kwa kutumia AI.


Kwa muda mrefu, kumekuwa na mjadala mkubwa na wasiwasi wa kimaadili kuhusu matumizi ya sauti za watu—hasa mastaa waliofariki—bila idhini ya wamiliki halali. Teknolojia kama 'deepfake' zimezua hofu ya matumizi mabaya ya sauti na sura za watu. Hata hivyo, ElevenLabs wamesema soko hili jipya linakuja na suluhu, wakitangaza kuwa linajengwa kwenye misingi ya "idhini, uwazi, na malipo ya haki" kwa wahusika wenyewe.


Mfumo huu unafanya kazi kama 'dalali' wa kidijitali. ElevenLabs inawaunganisha wafanyabiashara (kwa mfano, watengeneza matangazo, filamu, au michezo ya video) na wamiliki halali wa sauti hizo. Iwapo mhusika yuko hai, anatoa idhini yeye mwenyewe. Iwapo amefariki, kampuni inafanya makubaliano na familia, warithi, au taasisi zinazosimamia kazi na jina la marehemu. Baada ya makubaliano kufikiwa, ElevenLabs wanatumia teknolojia yao ya AI kutengeneza sauti bandia ambayo inafanana kikamilifu na sauti halisi.


Orodha ya awali iliyozinduliwa ina majina 28 ya watu maarufu sana duniani, wakiwemo walio hai na wale waliokwisha tangulia mbele za haki. Miongoni mwao ni wanasayansi wakubwa kama Thomas Edison (mvumbuzi wa balbu) na Alan Turing (anayetajwa kama baba wa kompyuta).


Pia, wapo waigizaji nguli wa filamu kama Sir Michael Caine (ambaye yuko hai na ametoa idhini), Judy Garland (aliyocheza 'The Wizard of Oz'), John Wayne, Burt Reynolds, na Laurence Olivier. Hata wanamichezo wa kihistoria kama nyota wa baseball Babe Ruth, na mwandishi maarufu Mark Twain wamejumuishwa.


Kwa wale ambao wamefariki, sauti zao za AI zimetengenezwa kwa kutumia rekodi zao za zamani za sauti walizowahi kurekodi wakati wa uhai wao. Hata hivyo, hii imezua swali jingine: Wengi wa watu hawa walifariki miongo mingi iliyopita, na ni watu wachache sana leo ambao wamewahi kusikia sauti zao halisi, jambo linalofanya iwe vigumu kuthibitisha usahihi kamili wa sauti hizo za AI.


Sir Michael Caine, mmoja wa waigizaji walio hai walioshiriki, ameupokea mpango huu kwa mikono miwili. Katika taarifa yake, alisema, "Hii siyo kuondoa sauti yangu, bali ni kuikuza na kuipa nguvu zaidi... Nimetumia maisha yangu yote kusimulia hadithi, na teknolojia hii itasaidia kizazi kijacho kusimulia hadithi zao wenyewe."


Hatua hii ya ElevenLabs inafungua mlango mpya kwa tasnia ya matangazo, ambapo sasa kampuni inaweza kumlipa kihalali mrithi wa mwanasayansi maarufu ili sauti ya AI ya mwanasayansi huyo itumike kuelezea bidhaa mpya ya kiteknolojia.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.