Katika hatua isiyo ya kawaida, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo wa 14, ambaye ameweka historia kama Papa wa kwanza kabisa kutoka nchini Marekani, ameamua kuingilia kati moja kwa moja kwenye mjadala moto unaoendelea duniani kote: kasi ya ukuaji wa Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI). Sauti yake inakuja wakati ambapo ulimwengu unashuhudia mashindano makali ya teknolojia hii, huku maswali kuhusu usalama na utu wa binadamu yakiachwa nyuma.
Akizungumza kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X (zamani Twitter) mnamo tarehe 7 Novemba, Papa Leo 14 alituma ujumbe wa wazi kwa wahandisi, watengenezaji wa programu, na wanasayansi wote wanaohusika na AI. Alisisitiza kuwa mchakato wa kubuni teknolojia hizi si suala la kompyuta na hesabu pekee, bali ni suala zito lenye "uzito wa ki-maadili na ki-roho."
Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi na kusema, "Ubunifu wa kiteknolojia unaweza kuwa njia ya kushiriki katika tendo la uumbaji la Mungu." Alionya kwamba, "Kila uamuzi unaofanywa katika mchakato wa usanifu hubeba maono kuhusu ubinadamu, na hivyo una uzito wake wa kimaadili." Kwa lugha rahisi, alimaanisha kuwa kila 'code' inayoandikwa na wahandisi hao ina uwezo wa kujenga au kubomoa mustakabali wa utu wa binadamu.
Papa aliwataka wataalamu hao wa kompyuta kuhakikisha "utambuzi wa kimaadili" unakuwa kiini cha kazi yao. Aliwasihi watengeneze mifumo inayoakisi "haki ya kweli, mshikamano kati ya watu, na heshima ya kweli kwa maisha."
Ujumbe huu mzito unakuja sambamba na hotuba yake ya hivi karibuni kwa washiriki wa 'Jukwaa la Wajenzi wa AI 2025' (Builders AI Forum 2025). Katika jukwaa hilo, alikemea vikali wazo la kwamba AI inapaswa kuendelezwa kwa malengo ya kibiashara na ya wawekezaji pekee. Alisema teknolojia hii inapaswa kutumika kwa manufaa ya wote, akitolea mifano kama "programu za elimu ya Kikristo, vifaa vya tiba vyenye huruma, na majukwaa ya ubunifu yanayosimulia hadithi za Kikristo kwa ukweli na uzuri."
Kauli ya Papa imekuja wakati makampuni makubwa ya teknolojia (Big Tech) na yale machanga (startups) yakichuana vikali kuona nani atakuwa wa kwanza, huku kukiwa na hofu kubwa kwamba masuala ya usalama, upotevu wa ajira, na athari za kiuchumi kwa binadamu zimepuuzwa. Tangu achaguliwe kuwa Papa mwezi Mei, Papa Leo 14 amekuwa akizungumzia waziwazi changamoto za AI, akisisitiza haja ya Kanisa kutoa "hazina ya mafundisho ya kijamii" ili kuongoza mapinduzi haya mapya ya viwanda.