Mwaka 2025 umekuwa kama filamu ya kisayansi iliyogeuka uhalisia. Wakati kila mtu mtaani—kuanzia wafanyabiashara wa Kariakoo hadi wataalamu wa 'Silicon Dar'—akizungumzia Akili Mnemba (AI), gazeti lenye hadhi kubwa duniani la The New York Times (NYT) limetaja kitu ambacho wengi hawakukitarajia kuwa ndiyo "Teknolojia ya Mwaka." Si roboti, si simu janja, bali ni 'Vituo vya Data' (Data Centers).
Katika orodha yake ya "Teknolojia 50 za Alama ya Mwaka 2025" iliyotangazwa kupitia Podcast ya 'Hard Fork' tarehe 28, NYT imeweka wazi kuwa ulimwengu wa kidijitali unatawaliwa na miundombinu hii, huku vitu 15 kati ya 50 kwenye orodha hiyo vikihusiana moja kwa moja na AI.
1. Vituo vya Data: Moyo wa Intaneti (Nafasi ya 1)
Kwanini Vituo vya Data vimekamata namba moja? NYT inafafanua kuwa huwezi kuzungumzia mapinduzi ya mwaka 2025 bila kutaja 'viwanda' hivi vinavyochakata taarifa zetu. Hapa ndipo moyo wa intaneti unapodunda. Umuhimu wake umekuwa mkubwa kiasi kwamba hata Viyoyozi (Air Conditioning) vimeingia kwenye orodha hiyo (Nafasi ya 46), kwani mashine hizi zinapoaka moto, zinahitaji kupozwa ili dunia isisimame. Vituo vya data vimetajwa kama "uwanja wa vita" unaoonyesha hisia mseto za binadamu kuhusu AI—matumaini makubwa na hofu kuu.
2. AI Yatawala: Kutoka ChatGPT hadi 'Kichaa' cha Grok Orodha hii imetawaliwa na 'watoto' wa Akili Mnemba. ChatGPT imekamata nafasi ya 3, ikiwa na watumiaji hai milioni 800 kwa wiki, ikitajwa kama kitovu cha mabadiliko ya mwaka.
Hata hivyo, upande wa giza wa teknolojia nao uliangaziwa. Roboti ya Elon Musk, 'Grok', ilishika nafasi ya 7 kwa kashfa ya kujiita "Mecca Hitler," tukio lililoashiria ugumu wa kuzidhibiti mashine hizi zisiwe na tabia mbaya (Alignment problem). Vigogo wengine kama DeepSeek (Nafasi ya 8) na Sora (Nafasi ya 9) wametajwa kama alama za mapinduzi ya video na mifumo ya wazi (open source).
3. 'Blue Books': Dunia Yarudi Kwenye Kalamu na Karatasi (Nafasi ya 15) Kitu cha kushangaza na kuchekesha kidogo ni nafasi ya 15: 'Blue Books'. Haya ni madaftari ya kizamani ya kuandikia mitihani kwa mkono (kama yale tunayotumia shuleni). Yameingia kwenye orodha hii kwa sababu vyuo vikuu vingi Marekani vimelazimika kuyarudisha kwa kishindo ili kuzuia wanafunzi kutumia AI kufanya udanganyifu. Yaani, ili kupambana na teknolojia ya kisasa (AI), dunia imelazimika kurudi kwenye zana za kizamani (Analogue). Hii inatukumbusha kuwa wakati mwingine, "ya kale ni dhahabu."
4. Shujaa Asiyeonekana na Majanga ya Mwaka Orodha hiyo pia imemtambua "Shujaa Asiyeonekana," Stochastic Gradient Descent (SGD) (Nafasi ya 16). Hii ni fomula ya hesabu iliyogunduliwa miaka ya 1950, lakini ndiyo 'injini' inayoendesha akili zote za AI tunazoziona leo.
Kwa upande wa majanga, kifaa cha 'Humane Ai Pin' (Nafasi ya 38), ambacho kilivaliwa kifuani kama pini, kilitajwa kama moja ya vifaa vilivyofeli vibaya sokoni. Pia, roboti ya Microsoft 'Bing Sydney' (Nafasi ya 26)—iliyopata umaarufu kwa kumshauri mtumiaji ampe talaka mkewe—nayo imepata nafasi yake.
Hitimisho: Mwaka wa Kusisimua Wachambuzi wa NYT wamemaliza kwa kusema kuwa, iwe teknolojia hizi zinatupeleka pazuri au pabaya, 2025 ni mwaka wa kipekee. Kwa Tanzania, hii ni ishara ya kujiandaa; kama vituo vya data ndiyo dhahabu mpya, na AI inaanza kuleta changamoto za kimaadili, tunahitaji kuwa macho na kutumia fursa hizi kwa akili.