Dunia ya teknolojia imeshuhudia 'mapinduzi ya kimya kimya' ambayo yanatazamiwa kubadilisha kabisa jinsi makampuni makubwa yanavyojenga miundombinu ya Akili Mnemba (AI). Kampuni mbili kubwa zinazotegemewa zaidi duniani kwa vipuri vya kompyuta, NVIDIA (wafalme wa GPU) na ARM (wafalme wa usanifu wa CPU), wameungana katika ushirikiano mpya unaolegeza masharti magumu yaliyokuwepo awali.
Kimsingi, makubaliano haya yanavunja ukuta mkubwa uliokuwepo. Hapo awali, ili kutumia teknolojia ya kasi ya ajabu ya NVIDIA inayoitwa 'NVLink' (teknolojia inayoruhusu chipu kuwasiliana kwa kasi ya umeme), ilikulazimu mara nyingi kutumia 'ubongo' (CPU) wa NVIDIA wenyewe. Ilikuwa kama vile ukitaka kutumia injini ya Ferrari, lazima ununue na bodi ya Ferrari.
Lakini sasa, ARM wametangaza kuingiza teknolojia hiyo ya 'NVLink Fusion' moja kwa moja kwenye mifumo yao ya 'Neoverse'. Hii ina maana gani? Sasa makampuni kama Google, Amazon, au Microsoft—ambayo yanapenda kutengeneza 'bongo' zao wenyewe (custom ARM CPUs)—yanaweza kuchukua CPU zao na kuziunganisha moja kwa moja na 'misuli' ya NVIDIA (GPUs) bila kikwazo chochote.
NVIDIA Yabadilisha Gia Angani
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanaona hatua hii kama ujanja mkubwa wa kibiashara wa NVIDIA. Wameamua "kukubali yaishe" upande wa kuuza CPU zao, ili walinde biashara yao kuu ya kuuza GPU. Kwa kuruhusu kila mtu atumie teknolojia yao ya uunganishaji (NVLink), NVIDIA wanahakikisha kuwa kila barabara ya data inaelekea kwenye GPU zao, bila kujali unatumia CPU ya nani.
Hii ni faida kubwa kwa ARM pia. Ushirikiano huu unawapa tiketi ya moja kwa moja kuingia kwenye soko la seva za AI, eneo ambalo limekuwa likikua kwa kasi ya roketi. Inatoa fursa kwa mataifa na makampuni kujenga miundombinu inayojitegemea (Sovereign AI) kwa gharama nafuu na bila utata wa kiufundi.
Intel na AMD Wana Hali Mbaya?
Wakati NVIDIA na ARM wakigonga glasi kusherehekea, washindani wao wakuu wanapata tumbo joto. Intel, ambayo imekuwa ikipambana kurudisha hadhi yake, sasa inakabiliwa na hatari ya kupoteza soko zaidi kwa ARM, kwani wateja hawatakuwa na sababu ya kung'ang'ania chipu za Intel.
Kwa upande wa AMD, hali ni ngumu zaidi. Kampuni hii inashambuliwa pande zote; kwenye GPU, CPU, na sasa hata kwenye teknolojia ya uunganishaji (interconnects). Hata kampuni ya Broadcom, ambayo inauza vifaa vya mawasiliano ya data, sasa inaona NVIDIA ikiingilia soko lake la 'standadi' za uunganishaji.
Muungano huu unatafsiriwa kama faida kwa 'Wababe wa Data' (Hyperscalers) kama Amazon na Google, lakini ni tishio la wazi kwa yeyote anayajaribu kushindana na himaya ya NVIDIA katika zama hizi za AI.