Kampuni ya akili mnemba (AI), Perplexity, imeingia rasmi kwenye uwanja wa ushindani wa vivinjari vya intaneti kwa kuzindua kivinjari chake kipya chenye nguvu ya AI kinachoitwa 'Comet'. Uzinduzi huu unaonekana kama hatua ya moja kwa moja kuleta ushindani kwa kivinjari kinachotawala soko, Google Chrome.
Kinachofanya Comet kuwa cha kipekee ni uwezo wake wa kutumia AI kurahisisha kazi za mtumiaji. Kipengele chake kikuu, 'Comet Assistant', kinaweza kusoma na kuelewa maudhui ya kurasa za wavuti ambazo mtumiaji anazitembelea na kisha kumsaidia kutekeleza majukumu mbalimbali. Kwa mfano, Perplexity inaeleza kuwa Comet inaweza kupanga mikutano, kutuma barua pepe, kufanya muhtasari wa ratiba, au hata kulinganisha bima mbalimbali kwa niaba ya mtumiaji, yote haya bila kulazimika kufungua kurasa nyingi tofauti.
Lengo kuu la Perplexity ni kuondoa usumbufu wa sasa wa kutumia vivinjari, ambapo mtumiaji hulazimika kufungua na kufunga ‘tabs’ nyingi, jambo linalopoteza umakini na muda.
Katika taarifa yake, kampuni hiyo ilisema, "Ingawa intaneti imekuwa kama ubongo wa pili wa mwanadamu, vifaa tunavyotumia kuifikia bado ni vya kizamani na vinatufunga kwenye milolongo ya ‘tabs’ na ‘links’. Comet inalenga kubadilisha mchakato huu kuwa mmoja, rahisi, na kubadili taratibu ngumu kuwa mazungumzo mepesi."
Hata hivyo, teknolojia hii ya hali ya juu inakuja na gharama yake. Kwa sasa, kivinjari cha Comet kinapatikana kwa watumiaji waliojisajili kwenye mpango wa malipo wa 'Perplexity Max', ambao unagharimu Dola 200 za Marekani (takriban Shilingi 520,000) kwa mwezi.
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanaona hatua hii kama jaribio la Perplexity kupunguza utawala wa Google Chrome. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Statcounter za mwezi Juni, Chrome inashikilia asilimia 68.3 ya soko la vivinjari duniani, hivyo Comet inakabiliwa na kibarua kigumu kujipenyeza sokoni.