Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, HaloPesa, imefungua ukurasa mpya wa burudani na zawadi kwa wateja wake kwa kumtambulisha balozi wake mpya wa kidijitali, 'Mr. Bonus'. Ujio wa mhusika huyu wa kidijitali unaashiria mwanzo wa kampeni kabambe iitwayo "Tamba na Bonasi," inayolenga kubadilisha miamala ya kila siku kuwa fursa za ushindi.
Kupitia kampeni hii, kila muamala unaofanywa na mteja wa HaloPesa—iwe ni kutuma pesa, kulipia bili, kununua bidhaa, au hata kununua umeme (LUKU)—sasa utakuwa na thamani ya ziada. Wateja watapata bonasi za papo kwa hapo na pia wataingizwa kwenye droo za kila siku, wiki, na mwezi, ambapo wanaweza kujishindia zawadi nono ya fedha taslimu hadi Shilingi Milioni 2.
Akielezea mkakati huu, Mkuu wa Idara ya Biashara wa HaloPesa, Happy Mzena, alisema kampuni inataka kila mteja ahisi msisimko na faida kila anapotumia huduma zao. "Mr. Bonus anawakilisha dhamira yetu ya kuongeza thamani. Hatutaki mteja afanye muamala tu, bali afurahie na apate fursa ya kushinda," alisema Mzena.
Naye Afisa Masoko, Aidat Lwiza, aliongeza kuwa lengo ni kufanya huduma za kifedha za kidijitali zivutie zaidi. "Tumeunda uzoefu wa kipekee ambapo Mr. Bonus analeta uhai na burudani, akihakikisha kila muamala unakuwa na msisimko wa ushindi," alifafanua. Lwiza aliwakumbusha wateja kuhusu unafuu wa HaloPesa, akitaja kuwa kutuma pesa kutoka HaloPesa kwenda HaloPesa kupitia App ni bure, kama ilivyo kwa ununuzi wa LUKU.
Katika kuhakikisha usalama wa wateja, HaloPesa imetoa tahadhari muhimu: washindi watapokea ujumbe mfupi kutoka kwa jina rasmi la 'HaloPesa' na simu za uthibitisho zitapigwa kupitia namba ya huduma kwa wateja, 100 pekee, ili kuepuka matapeli.