Marekani Yamnasa Mdukuzi wa China Aliyeiba Tafiti za COVID-19 na Kushambulia Kampuni 60,000

it | Thu Jul 10 2025


Marekani Yamnasa Mdukuzi wa China Aliyeiba Tafiti za COVID-19 na Kushambulia Kampuni 60,000

Mamlaka nchini Marekani imefanikiwa kumtia mbaroni raia mmoja wa China, Xu Zewei, anayetuhumiwa kutekeleza mashambulizi makubwa ya kimtandao kwa niaba ya serikali ya China. Kukamatwa kwake, kulikofanyika nchini Italia kufuatia ombi la Idara ya Sheria ya Marekani, kunafungua ukurasa mpya katika vita dhidi ya ujasusi wa kidijitali unaofanywa na mataifa makubwa.


Zewei, pamoja na mwenzake Zhang Yu ambaye bado anasakwa, wanakabiliwa na orodha ndefu ya makosa tisa. Mashtaka makuu dhidi yao ni pamoja na kufanya udukuzi na kuiba taarifa muhimu za tafiti za janga la COVID-19 kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Marekani mnamo Februari 2020. Kwa mujibu wa Idara ya Sheria, Zewei alikuwa akifanya kazi na kampuni ya Shanghai Powerock Network, ambayo inaaminika kuwa chombo kinachotekeleza operesheni za udukuzi kwa maslahi ya serikali ya Beijing.


Mbali na wizi wa tafiti za kisayansi, washtakiwa hawa wanahusishwa na shambulio la kihistoria la kimtandao lililoanza Machi 2021. Shambulio hili lililenga mifumo ya barua pepe ya kampuni inayojulikana kama 'Microsoft Exchange Server'. Hii ni mifumo ambayo kampuni na taasisi nyingi hutumia kwa mawasiliano yao ya ndani.


Kundi la wavamizi hawa, lililopewa jina la utani 'Hafnium', lilifanikiwa kupenyeza na kuingia kwenye mifumo ya barua pepe ya ndani ya zaidi ya kampuni 60,000 nchini Marekani. Wengi wa waathirika walikuwa ni wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), ambapo wavamizi waliweza kuiba taarifa nyeti kama vile barua pepe za siri za kampuni na orodha za anuani za wafanyakazi na wateja.


Uchunguzi unaonesha kuwa baada ya operesheni ya Hafnium, kundi hili lilibadili jina na kuanzisha mradi mpya wa udukuzi ujulikanao kama 'Silk Typhoon'. Watafiti wa usalama wa mtandao wanabainisha kuwa kundi hili sasa limeelekeza mashambulizi yake kwa mashirika makubwa zaidi ya kibiashara na hata taasisi za serikali, likiendeleza vitendo vya ujasusi wa kimtandao kwa kiwango cha juu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.