Sakata zito limeibuka katika viunga vya kampuni kubwa ya kutengeneza 'chip' za kompyuta duniani, Intel, baada ya mwajiriwa wao wa zamani kuamua 'kufunga virago na siri za kampuni'. Intel imemburuza mahakamani mhandisi wake wa zamani wa programu, Bwana Jinfeng Luo, ikimtuhumu kwa wizi wa kimkakati wa data nyeti sana, na sasa inadai fidia ya Dola za Kimarekani 250,000 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Milioni 685).
Kisa hiki kinachofanana na filamu za kijasusi kilianza Julai mwaka jana. Bwana Luo, ambaye alikuwa ameitumikia kampuni hiyo kwa uaminifu tangu mwaka 2014, alipewa barua ya kusitishiwa ajira mnamo Julai 7, huku siku yake ya mwisho kazini ikiwa imepangwa kuwa Julai 31. Inaonekana 'hasira ya mkizi' ilimwingia, na akaamua hatakubali kuondoka mikono mitupu.
Kulingana na hati za mashtaka, siku nane kabla ya kuaga rasmi, Luo alijaribu njia ya kizamani ya kuiba data kwa kuchomeka 'external hard drive' kwenye kompyuta yake ya ofisini. Kwa bahati nzuri, mifumo ya ulinzi ya Intel ilishtuka na kuzuia jaribio hilo. Hata hivyo, hakukata tamaa. Siku tano baadaye, alitumia ujanja wa kiteknolojia zaidi kwa kutumia mfumo wa uhifadhi wa mtandao (NAS) kukwepa walinzi wa kidijitali. Katika muda wa siku tatu mfululizo, anadaiwa kupakua mafaili takriban 18,000, mengine yakiwa na mhuri wa "SIRI NZITO" (Top Secret).
Kinachofanya kesi hii iwe ya kusisimua zaidi ni kwamba mtuhumiwa ameyeyuka kusikojulikana. Intel wanasema wamejaribu kila njia kumtafuta—kwa simu, barua pepe, na hata posta kwa zaidi ya miezi mitatu—bila mafanikio. Ni kama ameingia mitini jumla.
Tukio hili linakuja wakati mbaya kwa Intel, ambayo inapitia kipindi kigumu kiuchumi na imelazimika kupunguza maelfu ya wafanyakazi (takriban 15% ya nguvukazi yake) ili kujiweka sawa. Wizi huu unakumbushia tukio lingine la mwaka jana ambapo mhandisi mwingine alihukumiwa kwa kuiba siri za utengenezaji wa 'CPU' ili kumrahisishia kupata kazi mpya Microsoft.
Intel sasa wameiomba mahakama itoe amri ya kumtaka Luo arudishe vifaa vyote vya kielektroniki alivyonavyo na data zote alizoiba, huku wakisisitiza kuwa kitendo chake kimevunja sheria za shirikisho na za jimbo kuhusu ulinzi wa siri za biashara.