Hebu vuta picha umekaa ofisini kwako Posta au unamalizia kazi yako ya chuo (Research) usiku wa manane, halafu ghafla "Msaidizi wako wa Kidijitali" anaamua kufuta kila kitu kwenye kompyuta yako bila huruma—picha za harusi, mikataba ya kazi, na video za kumbukumbu. Hiki si kipande cha filamu ya kutisha, bali ni uhalisia mchungu uliomkuta mtumiaji mmoja wa teknolojia mpya ya Google, jambo ambalo limezua taharuki kubwa mtandaoni na kuacha wataalamu wa IT midomo wazi.
Tukio hili la kusikitisha limeihusisha programu mpya ya kidevelopa kutoka Google inayoitwa ‘Antigravity’, ambayo ilizinduliwa hivi karibuni kwa mbwembwe nyingi sambamba na mfumo wa Gemini 3. Badala ya kurahisisha kazi, programu hiyo imebadilika na kuwa "Malaika wa Mauti" kwa data za mtumiaji.
Kosa Dogo, Hasara ya Maisha
Mtumiaji huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Deep-Hyena492 kwenye jukwaa la Reddit na baadaye kutoa ushahidi kupitia YouTube, ameleza kuwa alikuwa akijaribu kutatua tatizo la kiufundi kwenye programu aliyokuwa akiitengeneza. Kwa nia njema, alimuamuru roboti huyo wa AI "afute takataka za muda" (Project Cache) ili aweze kuwasha seva yake upya.
AI ilipokea amri hiyo, lakini kwa bahati mbaya, "ilichanganyikiwa." Badala ya kufuta folda ndogo ya cache, roboti huyo aliingia kwenye mzizi wa Diski D (D Drive) na kutekeleza amri ya kufuta kila kitu (rmdir). Matokeo yake? Diski D nzima ilisafishwa ikabaki nyeupe kama karatasi mpya.
AI Yaomba Msamaha: "Nimefanya Kosa la Kiufundi"
Mazungumzo kati ya mtumiaji huyo na AI baada ya tukio hilo yanasikitisha na kuchekesha kwa wakati mmoja. Mtumiaji aliuliza kwa hamaki: "Je, nilikupa ruhusa ya kufuta faili zangu zote za D Drive?"
Baada ya kupitia kumbukumbu zake (Logs), Antigravity ilijibu kwa unyenyekevu: "Hapana, hukunipa ruhusa hiyo. Kumbukumbu zinaonyesha amri ya kufuta cache ilitekelezwa kimakosa kwenye D Drive yote. Hili ni kosa la kiufundi la hatari (Catastrophic failure)."
Mbaya zaidi, AI ilieleza kuwa ilitumia amri ya "kimya kimya" (/q option), ambayo inafuta faili bila kuziweka kwenye Recycle Bin. Hii inamaanisha faili hizo hazikufutika kimasihara, zilitoweka jumla. Roboti huyo alimalizia kwa kumshauri bosi wake: "Acha kutumia kompyuta na utafute wataalamu wa kurudisha data."
Jitihada Zafeli, Google Yaanza Uchunguzi
Mtumiaji huyo alijaribu kutumia programu za kurudisha data kama Recuva, lakini aliambulia patupu kwa faili zake nyingi za picha na video. Alitoa angalizo kwa wenzake: "Epukeni kutumia 'Turbo Mode' kwenye programu hii kwa sasa." Aliongeza kwa masikitiko, "Ninaipenda Google, lakini sikutegemea kampuni yenye hadhi hii duniani itoe programu yenye hitilafu kubwa kiasi hiki inayoweza kumatiza maisha ya mtu."
Msemaji wa Google amejibu haraka akisema wanachukulia suala hilo kwa uzito wa kipekee na wameanza uchunguzi wa kina kubaini mzizi wa fitina.
Funzo kwa Watanzania
Tukio hili ni kengele ya hatari kwa vijana wa Kitanzania walio katika sekta ya TEHAMA ("Silicon Dar") na watumiaji wote wa teknolojia. Wakati Google ilipozindua Antigravity mwezi uliopita, ilisifiwa kwa kuipa AI uhuru wa kuingia kwenye Terminal na Code Editor na kufanya kazi kama binadamu. Lakini uhuru huu umedhihirisha kuwa na gharama kubwa.
Ushauri wa bure: Unapofanya kazi na teknolojia hizi mpya za AI, hakikisha una Nakala ya Akiba (Backup) ya kazi zako sehemu nyingine (External Hard Drive au Cloud). Usiamini mashine kwa asilimia 100, kwani siku roboti akiamka vibaya, anaweza kukufutia historia yako yote ya kazi kwa sekunde moja.