Watafiti wa Chuo Kikuu cha Harvard na MIT wamefanikiwa kuunda kompyuta ya kiasi (quantum computer) ambayo inaweza kufanya kazi saa mbili mfululizo bila kuzimwa. Wanadai kuwa kithoria, mfumo huo unaweza kufanya kazi kwa muda usio na ukomo.
Uwezo wa kufanya kazi kwa saa mbili unaweza kuonekana kuwa mdogo ikilinganishwa na kompyuta za kawaida ambazo zinaweza kufanya kazi kwa miezi, lakini katika ulimwengu wa kompyuta ya kiasi, haya ni mafanikio makubwa. Kompyuta nyingi za kiasi zinazopatikana sasa hufanya kazi kwa milisekunde chache tu, na hata vifaa bora zaidi vinaweza kufanya kazi kwa sekunde 10 tu.
Mtafiti Tuo T. Wang alisisitiza kuwa jaribio hili linaonyesha uwezekano wa kuongeza muda wa uendeshaji wa kompyuta za kiasi. Alisema, "Bado tuna safari ndefu, lakini kwa majaribio haya, ramani ya jinsi ya kufika huko imekuwa wazi."
Kukabiliana na Tatizo la Upotevu wa Atomu
Tofauti kuu kati ya kompyuta za kawaida na kompyuta za kiasi ni jinsi zinavyohifadhi data. Kompyuta za kawaida zinaweza kuhifadhi data hata bila umeme, lakini kompyuta za kiasi hutumia chembechembe za qubit kuhifadhi na kuchakata habari. Tatizo kubwa katika kompyuta za kiasi ni upotevu wa atomu (atom loss), ambapo qubit hupotea, na kusababisha upotevu wa habari na makosa katika mfumo.
Kukabiliana na tatizo hili, watafiti wameunda mfumo wa optical lattice conveyor belt na zana za optical tweezers. Mfumo huu unaweza kudumisha qubit 3,000 huku ukiingiza atomu mpya 300,000 kwa sekunde. Hii inaondoa tatizo la kupoteza qubit. Wang alieleza kuwa, "Hata kama kuna uwezekano mdogo wa atomu kupotea, tunaweza kuibadilisha haraka kwa kuingiza atomu mpya bila kuathiri habari za kiasi zilizohifadhiwa." "Sasa hakuna mipaka ya kiasili kwa muda wa uendeshaji wa kompyuta ya kiasi," aliongeza.
Watafiti wanatabiri kuwa kompyuta ya kiasi inayoweza kufanya kazi kwa muda usio na ukomo inaweza kupatikana ndani ya miaka mitatu, ingawa wataalam wa kibiashara wanasema inaweza kuchukua miaka mitano au zaidi.
Kompyuta ya kiasi ina uwezo wa kuleta mapinduzi makubwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Cryptography, Fedha, na Tiba. Hata hivyo, watafiti walisisitiza kwamba haitakuwa rahisi kwa mtu binafsi kutumia kompyuta ya kiasi nyumbani au ofisini katika miaka 10 ijayo.