Bosi wa Usalama 'Atumbuliwa' Baada ya Kuonya Roboti ya Nyumbani Inaweza Kupasua Vichwa vya Watu

it | Mon Nov 24 2025


Bosi wa Usalama 'Atumbuliwa' Baada ya Kuonya Roboti ya Nyumbani Inaweza Kupasua Vichwa vya Watu

Dunia ya teknolojia imegubikwa na hofu mpya baada ya kampuni maarufu ya kutengeneza roboti zinazofanana na binadamu (humanoids), Figure AI, kuburuzwa mahakamani na aliyekuwa Mkuu wake wa Usalama wa Bidhaa. Kesi hii imefungua mjadala mzito kuhusu usalama wa mashine hizi ambazo zinaandaliwa kuishi na wanadamu majumbani, huku ikidaiwa kuwa kampuni hiyo iliweka faida mbele kuliko uhai wa watu.


Huko California, Marekani, Bwana Robert Grundel, ambaye alikuwa mhandisi mkuu wa usalama katika kampuni hiyo, amewasilisha mashtaka mazito katika Mahakama ya Shirikisho. Grundel anadai kuwa alifutwa kazi kienyeji mwezi Septemba—kitendo anachokiita ni "kisasi"—mara tu baada ya kuwasilisha ripoti ya kitaalamu iliyoonyesha kuwa roboti hizo ni hatari kiasi cha kuweza kuua.


"Ina Nguvu ya Kuvunja Fuvu la Kichwa"


Katika nyaraka za mahakama zilizovuja kupitia kituo cha habari cha CNBC, Grundel anadai kuwa alimwonya Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo (CEO), Brett Adcock, pamoja na wahandisi wengine wakuu kuwa roboti hiyo ina hitilafu zinazoweza kusababisha maafa.


Kwa lugha ya picha, Grundel alitoa mfano wa tukio la kutisha ambapo roboti hiyo ilipata hitilafu (malfunction) na kupiga mlango wa jokofu la chuma (steel fridge). Pigo hilo lilisababisha bonde la kina cha nchi 0.25 (sawa na sentimita 0.6). Wataalamu wanahoji, ikiwa chuma gumu kilibonyea kiasi hicho, je, fuvu la kichwa cha binadamu au mtoto mdogo lingepona?


Hofu hii inazidi kuwa kubwa hasa ikizingatiwa kuwa tofauti na roboti za viwandani ambazo hufanya kazi mbali na watu, Figure AI inalenga kutengeneza roboti za kusaidia kazi za nyumbani—kupika, kufanya usafi, na kucheza na watoto.


Ulaghai kwa Wawekezaji?


Mbali na hatari za kimwili, Grundel ameibua tuhuma za udanganyifu wa kibiashara. Anadai kuwa kampuni ilimwagiza kuandaa "Ramani ya Usalama" (Safety Roadmap) kwa ajili ya kuwaonyesha wawekezaji ili wapate pesa. Hata hivyo, baada ya kuwasilisha mpango madhubuti, mabosi zake walipunguza vipengele muhimu vya usalama ili kuifanya ripoti hiyo "ipendeze" machoni pa wenye pesa.


Grundel anasema alipoonya kuwa kitendo cha kuficha ukweli huo kinaweza kutafsiriwa kama "utapeli na udanganyifu," alionekana kama kigingi na mtu anayekwamisha mambo. Hapo ndipo alipooneshwa mlango wa kutokea kwa kisingizio cha "mabadiliko ya mwelekeo wa biashara."


Jibu la Kampuni na Vita ya Kisheria


Kama ilivyo ada, Figure AI wamekanusha vikali madai hayo. Msemaji wa kampuni hiyo amedai kuwa Grundel alifukuzwa kwa sababu ya "utendaji mbovu wa kazi" na si kwa sababu ya kufichua maovu. "Madai yake ni ya uongo na tutathibitisha hilo mahakamani," ilieleza taarifa ya kampuni.


Hata hivyo, mwanasheria wa Grundel, Robert Ottinger, amesema kesi hii ni mtihani mkubwa kwa tasnia ya roboti. "Sheria za California zinamulinda mfanyakazi anayetoa taarifa za hatari. Tunataka dunia ijue madhara ya kukimbilia sokoni na bidhaa ambazo hazijakamilika kwa sababu ya tamaa ya faida," alisisitiza Ottinger.


Angalizo kwa Mustakabali


Kesi hii imekuja wakati ambapo kampuni nyingi za teknolojia zinashindana kutengeneza roboti za majumbani. Wataalamu wa masuala ya maadili ya AI wanaonya kuwa kuingiza mashine zenye nguvu kubwa majumbani bila vipimo vya kutosha ni sawa na kufuga chui na kutegemea atakuwa mpole kama paka.


Wakati Watanzania tukifurahia maendeleo ya teknolojia, tukio hili linatukumbusha kuwa "haraka haraka haina baraka." Itachukua miaka mingi kabla ya kuwa na uhakika wa usalama wa kuishi na roboti hizi chumba kimoja, hasa kwa kuzingatia masuala ya faragha na usalama wa watoto.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.