Kampuni ya Apple, ambayo kwa muda mrefu ilionekana kusita kuingia moja kwa moja kwenye ushindani wa kutengeneza mifumo ya Akili Bandia (AI) ya mazungumzo, sasa imebadili mwelekeo na kufanya uamuzi wa kimkakati. Kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg, Apple imeunda timu mpya maalum kwa ajili ya kutengeneza mfumo wake wa AI wa utafutaji na mazungumzo utakaoshindana moja kwa moja na ChatGPT.
Timu hiyo mpya imepewa jina la 'Answers, Knowledge and Information (AKI)' na inaongozwa na Robby Walker, mtaalamu mwenye uzoefu wa kuendeleza msaidizi wa sauti wa Apple, Siri. Umuhimu wa timu hii unadhihirishwa na ukweli kwamba itakuwa ikiripoti moja kwa moja kwa Mkuu wa Kitengo cha AI cha Apple, John Giannandrea. Hii ni ishara tosha kwamba Apple sasa inataka kujenga teknolojia hii muhimu yenyewe, badala ya kutegemea washirika wa nje pekee.
Tatizo la Siri na Mkakati Mpya
Hatua hii inakuja wakati ambapo mipango ya kuifanyia marekebisho makubwa Siri imekumbwa na changamoto. Ingawa Apple bado inaendelea na ushirikiano wake na OpenAI ili kuunganisha baadhi ya uwezo wa ChatGPT kwenye Siri, uzinduzi wa Siri mpya na iliyoboreshwa umeahirishwa hadi mwaka ujao.
Mkuu wa Uhandisi wa Programu wa Apple, Craig Federighi, alikiri mbele ya wafanyakazi kuwa jaribio la awali la kuchanganya mfumo wa zamani wa amri wa Siri na teknolojia mpya ya AI "halikufikia viwango vya ubora vya Apple," na hivyo kuhitaji mabadiliko ya kimuundo.
Ahadi ya Tim Cook na Mkakati wa 'Mvumbuzi wa Baadaye'
Katika mkutano usio wa kawaida na wafanyakazi wote, Mkurugenzi Mtendaji, Tim Cook, alisisitiza umuhimu wa AI. "AI ni mapinduzi yaliyo sawa au hata makubwa kuliko intaneti, simu janja (smartphone), na 'apps'," alisema Cook. "Apple lazima ifanikiwe katika hili, na tuko tayari kuwekeza."
Alikumbushia mkakati wa kihistoria wa Apple: "Sisi huwa si wa kwanza sokoni, lakini siku zote huleta mabadiliko ya kweli yanayobadili mchezo." Hii ina maana kwamba Apple haikimbilii kutoa bidhaa, bali inalenga kuingia sokoni na bidhaa yenye ubora wa hali ya juu na inayotoa uzoefu bora kwa mtumiaji, na hivyo kubadilisha kabisa soko hilo.
Changamoto za Ndani
Hata hivyo, safari hii si rahisi. Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, takriban wataalamu wanne muhimu kutoka timu ya msingi ya AI ya Apple wamehama na kujiunga na mshindani wao, Meta. Hii inaonyesha ushindani mkali wa kupata na kuhifadhi wataalamu wa AI. Pia, inaripotiwa kuwa kiongozi wa timu hii mpya ya AKI, Robby Walker, aliwahi kuukosoa mradi wa Siri ulioahirishwa, akiuita kuwa "mbaya na wa aibu," kuonyesha presha kubwa iliyopo ndani ya kampuni ya kufanya vizuri.
Licha ya changamoto hizi, Apple sasa imeweka wazi nia yake ya kuingia kwa nguvu kamili katika uwanja wa AI ya mazungumzo, na ulimwengu wa teknolojia unasubiri kuona kama wataweza tena kurudia historia yao ya "kuchelewa lakini kufanikiwa."