Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema yuko tayari kuachia madaraka endapo hilo litawezesha nchi yake kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Kauli hiyo ameitoa wakati Ukraine ikiadhimisha miaka mitatu tangu ilipovamiwa na Urusi mnamo Februari 24, 2022.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Zelensky alisisitiza kuwa hana tamaa ya kushikilia madaraka kwa muda mrefu, lakini kipaumbele chake kwa sasa ni usalama wa Ukraine.
"Iwapo kuondoka kwangu madarakani kutaharakisha mchakato wa Ukraine kujiunga na NATO na kuleta amani, basi niko tayari kufanya hivyo," alisema Zelensky alipoulizwa kuhusu mustakabali wake wa kisiasa.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kumuita Zelensky *"dikteta"*. Hata hivyo, Zelensky alijibu kwa utulivu, akisema, "Sikuudhika na kauli hiyo, lakini dikteta angeudhika." Alisisitiza kuwa alichaguliwa kidemokrasia mnamo Mei 2019 na anaendelea kuheshimu misingi ya demokrasia.
Sheria za Ukraine zinakataza kufanyika kwa uchaguzi wa kitaifa wakati wa vita, jambo ambalo limezuia uchaguzi wa rais kufanyika tangu uvamizi wa Urusi uanze.
Katika kuonyesha mshikamano na Ukraine, viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuwasili Kyiv leo kwa mazungumzo kuhusu usalama wa taifa hilo. Miongoni mwa viongozi hao ni Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez, Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, na Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen.