Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti kuwa boti nne zilizokuwa zikiwasafirisha wahamiaji zimezama katika Bahari ya Shamu, kati ya Yemen na Djibouti, na kusababisha vifo vya angalau watu wawili huku wengine 186 wakiripotiwa kupotea.
Kwa mujibu wa msemaji wa IOM, Tamim Elian, boti mbili kati ya hizo zilipata ajali mnamo Machi 6 karibu na pwani ya Yemen. "Katika ajali hiyo, mabaharia wawili waliokolewa, lakini wahamiaji 181 pamoja na mabaharia wa Yemen watano bado hawajapatikana," alisema.
Boti nyingine mbili pia zilizama karibu na Djibouti muda mfupi baadaye. Katika ajali hiyo, miili ya wahamiaji wawili ilipatikana, lakini abiria waliobaki waliokolewa.
Njia Hatari ya Wahamiaji Kati ya Afrika na Kati ya Mashariki
Kwa mujibu wa IOM, tangu mwanzoni mwa mwaka 2024 pekee, takriban wahamiaji 558 wamepoteza maisha wakiwa wanajaribu kuvuka kutoka Pembe ya Afrika hadi Yemen kupitia Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden. Njia hii imeendelea kuwa mojawapo ya safari hatari zaidi kwa wahamiaji wanaotafuta fursa za maisha bora Mashariki ya Kati.
Licha ya hatari ya mawimbi makali na hali mbaya ya anga, maelfu ya wahamiaji, wengi wao wakiwa kutoka Ethiopia na Somalia, wanaendelea kujaribu safari hii wakitarajia kufika Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba.
Ajali hizi zinatilia mkazo changamoto kubwa za wahamiaji, zikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, ukosefu wa usalama barabarani, na hali mbaya ya maisha inayopelekea watu wengi kuhatarisha maisha yao baharini.