Hali ya wasiwasi imeongezeka katika njia muhimu ya biashara ya Bahari ya Shamu baada ya kundi la waasi wa Kihouthi nchini Yemen kudai kuzamisha meli ya pili ya mizigo ndani ya siku chache. Katika tukio la hivi karibuni, meli ya 'Eternity C', inayomilikiwa na kampuni ya Ugiriki na iliyopeperusha bendera ya Liberia, ilishambuliwa na kuzamishwa, huku kukiwa na hofu ya vifo vya watu kadhaa.
Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi, Yahya Saree, alitangaza shambulio hilo kupitia video iliyorekodiwa, akidai kuwa wapiganaji wao waliwaokoa baadhi ya mabaharia na kuwapa huduma za kimatibabu. Hata hivyo, taarifa kutoka kwa maafisa wa usalama walioshiriki katika operesheni ya uokoaji zinaonyesha picha tofauti na ya kutisha: watu wanne wamethibitishwa kufariki, sita wameokolewa, na wengine 15 bado hawajulikani walipo.
Shambulio dhidi ya 'Eternity C' lilitokea kati ya usiku wa Julai 7 na alfajiri ya Julai 8, katika eneo la takriban kilomita 94 kutoka bandari ya Hodeidah inayodhibitiwa na Wahouthi. Inaarifiwa meli hiyo ilivamiwa na mashua ndogo zilizofyatua risasi pamoja na mashua isiyo na rubani iliyosheheni vilipuzi.
Tukio hili limekuja siku chache tu baada ya Wahouthi kushambulia na kuzamisha meli nyingine iitwayo 'Magic Seas' mnamo Julai 6. Kundi hilo lilitoa video ya propaganda ikionyesha wapiganaji wao wakiipanda meli hiyo, kutega vilipuzi, na kisha kuilipua. Walidai kuwa meli hiyo ililengwa kwa sababu kampuni inayoimiliki iliendelea kufanya biashara na bandari za Israel. Mabaharia wote 22 wa 'Magic Seas' waliokolewa na meli nyingine ya kibiashara.
Kurejea kwa mashambulizi haya mfululizo kumezua upya hofu na taharuki katika sekta ya usafirishaji baharini, kwani Bahari ya Shamu ni njia muhimu kwa biashara ya kimataifa.
Wahouthi walianza kampeni yao ya mashambulizi mnamo Novemba 2023, wakidai kuwa wanafanya hivyo kuwaunga mkono Wapalestina kufuatia kuanza kwa vita katika Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba 2023. Tangu wakati huo, wameshambulia zaidi ya meli 100, wakizamisha mbili na kuteka moja kabla ya matukio haya ya sasa. Ingawa walikuwa wamepunguza mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara mapema mwaka huu wa 2025 wakati mazungumzo ya amani yalipokuwa yakiendelea, wameendelea kurusha makombora kuelekea Israel na sasa wamerejea kwa kishindo katika kushambulia meli.