Serikali ya Marekani imeanza juhudi za kutuliza hali baada ya anguko kubwa la soko la hisa kutokana na wasiwasi kuhusu sera za ushuru za Rais Donald Trump. White House imesisitiza kuwa ingawa hatua za Trump zinaweza kuongeza hali ya kutokuwa na uhakika kwa muda mfupi, zitakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa muda mrefu.
White House: Soko la Hisa Linareact Kupita Kiasi
Afisa mmoja wa White House alisema kuwa mwelekeo wa soko la hisa haumaanishi taswira halisi ya hali ya uchumi. "Kuna tofauti kubwa kati ya hisia za soko na uelewa wetu wa hali halisi ya sekta mbalimbali za uchumi," alisema afisa huyo.
Msemaji wa White House, Kush Desai, aliongeza kuwa sera za Trump kuhusu ushuru, kupunguza masharti ya biashara, na kuimarisha sekta ya nishati ya Marekani tayari zimesababisha ahadi za uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka kwa makampuni makubwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Uchumi la Taifa (NEC), Kevin Hassett, alieleza kuwa ingawa data za robo ya kwanza ya mwaka zilionesha changamoto, uchumi wa Marekani unatarajiwa kuimarika zaidi katika robo ya pili kutokana na athari za kupunguzwa kwa kodi.
Trump Kukutana na Wakuu wa Makampuni
Rais Trump anatarajiwa kukutana na wakuu wa makampuni makubwa na benki tarehe 11 Machi kupitia taasisi ya Business Roundtable, shirika linalojumuisha zaidi ya wakurugenzi wakuu wa kampuni 200 zinazowakilisha sekta mbalimbali za uchumi wa Marekani.
Kikao hicho kitashirikisha viongozi wakuu wa kampuni kama vile Jamie Dimon wa JP Morgan na Jane Fraser wa Citigroup, ambapo Rais Trump atatoa msimamo wake kuhusu uchumi na sera za ushuru.
Elon Musk: "Hali Itakuwa Shwari Muda Mrefu"
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tesla, Elon Musk, amekiri kuwa kampuni yake inakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kushuka kwa thamani ya hisa zake kwa asilimia 15.4.
Musk, ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali katika utawala wa Trump, alitetea hatua za serikali za kupunguza matumizi na kupunguza ajira serikalini. Alisema hatua hizo ni muhimu kwa sababu kuna matumizi yasiyo ya lazima na udanganyifu serikalini.
Pamoja na changamoto hizo, Musk alisisitiza kuwa Tesla itaendelea kuimarika muda mrefu na kwamba historia imeonesha kuwa hisa za kampuni hiyo zimepata misukosuko mara nyingi kabla ya kuimarika tena.
Ripoti za kifedha kutoka kwa UBS na Baird zinaonesha kuwa Tesla ilikumbwa na kushuka kwa mauzo katika soko la Marekani na kimataifa katika miezi ya kwanza ya mwaka huu, hali iliyosababisha wawekezaji kuwa na wasiwasi zaidi.
Hata hivyo, Musk aliwahakikishia wawekezaji kuwa kampuni yake iko imara na itaendelea kustawi licha ya changamoto za sasa.