Hali ya taharuki imetawala jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil, kufuatia operesheni kali ya kijeshi iliyoendeshwa na polisi dhidi ya moja ya magenge hatari zaidi nchini humo. Operesheni hiyo, iliyofananishwa na vita kamili, imeacha takribani watu 121 wakiwa wamepoteza maisha, ikiwa ni pigo kubwa kwa genge la 'Comando Vermelho' (CV).
Taarifa kutoka kwa serikali ya jimbo la Rio de Janeiro zimethibitisha kuwa mapambano hayo makali yaliyodumu kwa siku kadhaa yalilenga kusambaratisha mtandao huo wa uhalifu. Katika idadi hiyo kubwa ya vifo, maafisa wanne wa polisi pia wamo miongoni mwa waliopoteza maisha wakitekeleza majukumu yao.
Ukubwa wa operesheni hii ulidhihirishwa na idadi ya askari na vifaa vilivyotumika. Zaidi ya askari polisi na maafisa usalama 2,500 walishiriki. Ili kukabiliana na upinzani mkali kutoka kwa wahalifu hao, mamlaka zilitumia zana nzito za kivita, ikiwemo helikopta mbili, magari 32 ya deraya, na magari maalum 12 ya mbinu za kivita yaliyoundwa kwa ajili ya kubomoa vizuizi na ngome za wahalifu hao.
Kando na idadi ya vifo, polisi walifanikiwa kupata ushindi mkubwa kwa kufumua ghala la silaha za wahalifu. Mkuu wa Polisi wa Rio de Janeiro, Felipe Kuri, alieleza kuwa walikuta "ghala la silaha ambalo ungetarajia kuliona kwenye uwanja wa vita." Miongoni mwa silaha zilizokamatwa ni bunduki za kivita za kisasa, ikiwemo AK-47.
Serikali ya jimbo ilitangaza kuwa thamani ya silaha zote zilizokamatwa inafikia takribani Reais za Brazil milioni 12.8, ambazo ni sawa na Shilingi za Kitanzania zipatazo Bilioni 5.9. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya silaha hizo ziliingizwa nchini humo kimagendo kutoka nchi kama vile Argentina, Peru na hata Urusi, jambo linaloonyesha ukubwa wa mtandao huu wa kimataifa.
Mamlaka zimekuwa zikitetea uhalali wa kutumia nguvu kubwa kiasi hicho. Polisi walitoa maelezo kupitia mitandao ya kijamii wakieleza kuwa genge la CV limekuwa likitanua himaya yake kwa kasi katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Inakadiriwa kuwa genge hili linahusika na usafirishaji wa takribani tani 10 za dawa za kulevya kila mwezi. Zaidi ya hayo, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Rio ilisema kuwa genge hilo linahusishwa na wastani wa tukio moja la mauaji kila siku katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, operesheni hiyo imezua hisia mseto. Baadhi ya familia za waathirika zimefanya maandamano mitaani, zikishutumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kufanya "mauaji ya papo kwa papo." Licha ya malalamiko hayo, inaonekana sehemu kubwa ya raia wa Brazil wanaunga mkono hatua hizo. Kura ya maoni ya haraka iliyofanywa na kituo cha habari cha G1 ilionyesha kuwa asilimia 57 ya wananchi walikubaliana na kauli ya Gavana wa jimbo, Cláudio Castro, kwamba operesheni hiyo ilikuwa ya mafanikio makubwa. Hali hii imeonekana kuongeza umaarufu wa kisiasa wa gavana huyo.