Polisi Mbeya Yakama Watu 342 kwa Dawa za Kulevya, Mauaji

culture | Thu Apr 03 2025


Polisi Mbeya Yakama Watu 342 kwa Dawa za Kulevya, Mauaji

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewakamata watu 342 kwa tuhuma za kuhusika na dawa za kulevya. Kati ya hao, wanaume ni 329 na wanawake ni 13. Dawa za kulevya zilizokamatwa ni pamoja na bangi yenye uzito wa kilogramu 1,450, gramu 517, na miche 653.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Benjamin Kuzaga, alitoa taarifa hiyo wakati akizungumzia mafanikio ya jeshi hilo katika miaka minne ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.


Alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni, misako, na doria zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.


Kamanda Kuzaga alitaja aina nyingine za dawa za kulevya zilizokamatwa kuwa ni heroine yenye uzito wa gramu 19.2, ambapo watuhumiwa sita walikamatwa (wanaume wanne na wanawake wawili). Pia, mirungi yenye uzito wa kilogramu tatu ilikamatwa kutoka kwa mwanaume mmoja.


Akizungumzia mafanikio ya kesi mahakamani, Kamanda Kuzaga alisema kuwa watuhumiwa saba walipatikana na hatia ya kunyongwa hadi kufa kutokana na matukio ya mauaji.


"Watuhumiwa 23 wa matukio ya kubaka na kulawiti walipatikana na hatia ya kifungo cha maisha gerezani. Watuhumiwa 21 wa matukio ya unyang'anyi wa kutumia silaha/nguvu walipatikana na hatia ya kifungo cha jela miaka 30, na 133 wa mtandao wa wizi kwa njia ya mtandao walikamatwa," alisema Kamanda Kuzaga.


Aliongeza: "Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tunajivunia mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. Samia Suluhu Hassan, katika nyanja mbalimbali, ikiwamo ya rasilimali watu, vifaa na majengo, katika kuzuia na kutanzua uhalifu pamoja na kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani."

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.