Kumezuka mzozo mkubwa wa kibiashara na kidiplomasia kati ya miamba miwili ya Asia, Japan na Vietnam. Chanzo cha mzozo huu ni uamuzi wa ghafla wa Serikali ya Vietnam kutangaza mpango kabambe wa kuanza kupiga marufuku pikipiki zote zinazotumia injini za mafuta (petroli) kuanzia mwaka ujao wa 2025.
Hatua hii, ambayo inalenga kuanzia katika jiji kuu la Hanoi, imeipandisha hasira serikali ya Japan. Kampuni za Kijapani, hasa Honda na Yamaha, ndizo wafalme wasiopingika wa soko la pikipiki nchini Vietnam kwa miongo kadhaa.
Japan haikukaa kimya. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ubalozi wa Japan mjini Hanoi tayari umetuma barua rasmi ya kidiplomasia kwa mamlaka za Vietnam mwezi Septemba, ukiitaka serikali hiyo kufikiria upya uamuzi huo. Katika barua hiyo, Japan imeonya kuwa mabadiliko hayo ya ghafla na yasiyokuwa na maandalizi ya kutosha yatasababisha "mshtuko mkubwa" kwa mfumo mzima wa kiuchumi na viwanda. Wanaeleza kuwa mtandao wa wauzaji (dealers), wasambazaji wa vifaa na 'spea', pamoja na mnyororo mzima wa ugavi utasambaratika.
Mpango wenyewe wa Vietnam, uliotangazwa na Waziri Mkuu Pham Minh Chinh mwezi Julai, unaonekana kuwa na nia njema kwa juu. Kuanzia katikati ya mwaka 2025, jiji la Hanoi litapiga marufuku kabisa uendeshaji wa pikipiki za mafuta. Sababu rasmi inayotolewa ni jitihada za kupambana na viwango vya kutisha vya uchafuzi wa hewa jijini humo. Mpango huo unatarajiwa kusambaa katika miji mingine mikuu nchini humo ifikapo mwaka 2028, huku jiji la kibiashara la Ho Chi Minh nalo likitafakari kuchukua hatua kama hiyo.
Ili kuelewa uzito wa mzozo huu, ni lazima kuelewa ukubwa wa soko. Biashara ya pikipiki nchini Vietnam ina thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 4.6 (sawa na takriban Shilingi Trilioni 12 za Kitanzania) kwa mwaka, likiwa ni moja ya masoko makubwa zaidi duniani. Katika nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 100, inakadiriwa asilimia 80 ya watu wote wanamiliki pikipiki.
Na hapa ndipo penye kiini cha tatizo kwa Japan: Kampuni ya Honda pekee inashikilia asilimia 80 ya soko lote. Hali hii ni sawa na hapa kwetu Tanzania; kama ambavyo neno 'Bajaj' au 'Boxer' linavyoweza kutumika kumaanisha 'bodaboda', nchini Vietnam neno 'Honda' ndilo jina lenyewe la pikipiki.
Pigo kwa Honda limeanza kuonekana hata kabla ya marufuku kuanza. Mauzo ya kampuni hiyo mwezi Agosti yaliporomoka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na mwezi uliopita. Hali iliendelea kuwa mbaya mwezi Septemba. Hii ni hasara kubwa kwa Honda, ambayo baada ya kupitwa katika soko la magari ya umeme, imekuwa ikitegemea sana faida kutokana na biashara ya pikipiki.
Chama cha Watengenezaji Pikipiki nchini Vietnam (VAMM), kinachowajumuisha Honda, Yamaha, na Suzuki, kimepinga vikali mpango huo. Kimeonya kuhusu uwezekano wa "mporomoko wa mnyororo wa ugavi na kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira." Chama hicho kinakadiria kuwa zaidi ya wauzaji 2,000, viwanda vidogo vya spea 200, na mamia kwa maelfu ya wafanyakazi watapoteza vibarua vyao. Wanadai kuwa ili mabadiliko kama hayo yafanyike, wanahitaji muda wa maandalizi wa angalau miaka miwili hadi mitatu.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaona kuwa nyuma ya pazia la 'mazingira', kuna mkakati mwingine mkubwa wa kiuchumi. Vietnam inaonekana kutumia suala la hewa chafu kama kisingizio cha kukuza viwanda vyake vya ndani vya pikipiki za umeme. Nchi hiyo inaweka nguvu kubwa kuzipaisha chapa zake za kizalendo kama vile VinFast na Selex Motors. Serikali imeanza kutoa ruzuku (subsidy) kwa wananchi watakaonunua pikipiki za umeme na inajenga kwa kasi miundombinu ya vituo vya kuchaji. Mkakati huu unaonekana kufanikiwa; katika robo ya pili ya mwaka huu, mauzo ya pikipiki za umeme za VinFast yalipanda kwa asilimia 55.
Sasa Serikali ya Vietnam ipo njia panda. Japan ni mmoja wa wawekezaji wakubwa na wafadhili muhimu zaidi nchini Vietnam. Waziri Mkuu Chinh, alipokutana na wafanyabiashara wa Kijapani mwezi Agosti, alijaribu kuwapooza kwa kusema "atatafuta mpango bora wa utekelezaji." Vietnam sasa inakabiliwa na mtihani wa jinsi ya kusawazisha ajenda yake ya mazingira, mkakati wake wa kulinda viwanda vya ndani, na wakati huo huo kulinda uhusiano wake wa kidiplomasia na mwekezaji wake mkuu.