Viongozi wa Makanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENCO) pamoja na Kanisa la Kristo (ECC), mnamo Februari 12, 2025, walikutana na wanamgambo wa kundi la waasi wa AFC-M23 kwa mazungumzo ya kuimarisha juhudi za amani nchini humo.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika Hoteli ya Serena mjini Goma, ambako viongozi hao waliwapongeza wanamgambo wa M23 kwa juhudi zao za kudumisha utulivu katika mji huo walioutwaa hivi karibuni. Viongozi wa makanisa walisema kuwa kwa mara ya kwanza Goma inafanya kazi saa 24 bila matukio ya wizi wa kutumia silaha au vurugu, jambo ambalo lilikuwa tofauti na matarajio ya wengi.
Kabla ya kukutana na M23, viongozi hao walifanya mazungumzo na Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, kujadili hali ya usalama na njia za kudumisha amani katika taifa hilo lenye changamoto za kiusalama.
Wakati huo huo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imechukua hatua kali dhidi ya Rwanda, kwa kufunga anga yake kwa ndege zote za kiraia na za serikali zilizosajiliwa nchini Rwanda. Hatua hiyo ilitangazwa mapema leo na shirika la habari la Agence Congolaise de Presse, ikiwa ni sehemu ya kujibu tuhuma za Rwanda kufadhili mashambulizi ya wanamgambo wa M23.
M23 wamehoji hatua hiyo, wakisema, "Kuzuia ndege za Rwanda kutumia anga ya DRC ni mkakati wa kiulinzi au michezo ya kisiasa tu? Kukata ufikiaji wa anga hakutasuluhisha mizozo zaidi. Je, Kinshasa inathibitisha ujasiri au inakosa washauri bora?"
Mamlaka ya uwanja wa ndege wa Kongo imetoa marufuku rasmi kwa ndege zote za kiraia na za serikali zilizosajiliwa Rwanda, au zile zilizosafiri kutoka Rwanda, kupaa au kutua katika anga ya DRC kutokana na hali ya ukosefu wa usalama unaosababishwa na vita.
Katika mapigano ya hivi karibuni kati ya wanamgambo wa M23 na jeshi la Kongo, takribani wanajeshi 20 wa kikosi cha kulinda amani waliuawa, wakiwemo wanajeshi 14 kutoka Afrika Kusini. Mabaki ya miili ya wanajeshi hao yanatarajiwa kurejeshwa Afrika Kusini siku ya Alhamisi.
Hatua za serikali ya DRC zinaongeza mvutano katika eneo hilo, huku juhudi za kurejesha amani zikiendelea kupitia mazungumzo ya kidiplomasia.