Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria (SDF), ambavyo vinaongozwa na Wakurdi, vimeanza kujiondoa kutoka maeneo ya mpaka na Uturuki.
Shirika la habari la taifa la Syria, SANA, liliripoti jana kuwa magari yaliyokuwa yamebeba wapiganaji wa SDF yalionekana yakisafiri kupitia mji wa Aleppo kuelekea upande wa mashariki wa Mto Euphrates. Hii ilifanyika chini ya usimamizi wa serikali ya mpito.
Shirika la habari la Uturuki la Anadolu liliripoti mnamo Aprili 3 kuwa takriban watu 250 waliachiliwa huru huko Aleppo kupitia kubadilishana wafungwa kati ya serikali ya mpito na SDF.
Hatua hizi zinatokana na makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita kati ya serikali ya mpito ya Syria na SDF, ambapo pande hizo mbili zilikubaliana kuunganisha wapiganaji na muundo wa SDF katika jeshi la kawaida la Syria.
Kufuatia makubaliano haya, kuna matumaini kuwa eneo la mpaka wa kaskazini mwa Syria, ambalo limekuwa eneo la mapigano kati ya jeshi la Uturuki na vikosi vya wanamgambo wa Kikurdi, litakuwa na utulivu zaidi.
Uturuki inaiona SDF kuwa na uhusiano na Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi (PKK) na Vitengo vya Ulinzi vya Watu wa Kikurdi (YPG), ambavyo Uturuki inaviorodhesha kama mashirika ya kigaidi. Kwa miaka kadhaa, Uturuki imekuwa ikifanya operesheni za kijeshi dhidi ya makundi haya.
Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 13, SDF ilikuwa moja ya vikosi vya upinzani vilivyopigana dhidi ya utawala wa kiimla wa Bashar al-Assad. Tofauti na Uturuki, Marekani inaiona SDF kama mshirika muhimu katika vita dhidi ya kundi la Islamic State (IS) Mashariki ya Kati.
Baada ya utawala wa Assad kuanguka na serikali ya mpito kuingia madarakani kufuatia mashambulizi yaliyoongozwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) mnamo Desemba mwaka jana, mapigano ya mara kwa mara yaliendelea kutokea kaskazini mashariki mwa Syria kati ya SDF na vikosi vya waasi vinavyoungwa mkono na Uturuki.
Kwa kuwa waasi wanaoungwa mkono na Uturuki walishiriki katika mashambulizi ya HTS, serikali ya Uturuki kwa sasa inafanya kazi kwa karibu na serikali ya mpito ya Syria inayoongozwa na Rais wa muda Ahmed al-Sharaa, ambaye anatoka katika safu za uongozi wa HTS. Ushirikiano huu unawezesha Uturuki kuendelea kuweka wanajeshi wake nchini Syria na kujenga kambi za kijeshi.
Wakati huohuo, wito uliotolewa mnamo Februari na mwanzilishi wa PKK, Abdullah Öcalan, akiwa gerezani, akitaka kusitishwa kwa mapambano ya silaha dhidi ya Uturuki na kuvunjwa kwa PKK, umeleta sura mpya katika mzozo wa muda mrefu kati ya Uturuki na PKK.