Mauzo ya magari ya umeme ya Tesla yameendelea kuporomoka katika masoko mbalimbali duniani, huku Australia ikishuhudia kushuka kwa mauzo kwa asilimia 72 mnamo Februari. Kupungua kwa mahitaji ya magari ya umeme, ushindani mkali kutoka kwa makampuni ya China, na utata unaomzunguka mwanzilishi wa Tesla, Elon Musk, vinatajwa kuwa sababu kuu za hali hii.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka The Guardian Australia, mauzo ya Tesla Model 3, ambayo ni gari lake la bei nafuu zaidi na lililokuwa likiongoza kwa mauzo, yameshuka kwa asilimia 81 katika soko la Australia. Hii ni dalili wazi ya mabadiliko makubwa katika mtazamo wa watumiaji kuhusu bidhaa za Tesla.
Licha ya ushindani mkali kutoka kwa makampuni ya Kichina ambayo yanauza magari ya umeme kwa bei nafuu, na kupungua kwa mahitaji ya magari kwa ujumla, wachambuzi wanahoji kuwa kuporomoka kwa mauzo ya Tesla kunahusiana pia na msimamo tata wa Musk.
Musk, ambaye kwa sasa anaonekana kama mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump, amekosolewa vikali kwa vitendo vyake vya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuonekana akifanya salamu inayodhaniwa kuwa ya Kinasisti (Nazi) katika hafla ya kusherehekea ushindi wa Trump mnamo Januari.
Katika Australia, hasira dhidi ya Musk inaendelea kuongezeka. Mkaazi wa Sydney, Jess, ambaye anaendesha Tesla Model Y aliyopata kupitia mpango wa ukodishaji wa kampuni ya mumewe, alisema, "Niliona picha ya Musk akifanya ishara hiyo, na nilitaka kuuza gari yangu mara moja. Sasa najisikia aibu kuliendesha." Hata hivyo, kutokana na mkataba wa ukodishaji usio rahisi kusitisha, aliamua kubandika stika kwenye gari lake iliyoandikwa, "Nililinunua kabla Elon hajaanza kupoteza mwelekeo."
Mteja mwingine wa Tesla alisimulia kuwa alichukizwa na Musk kiasi cha kuamua kuuza gari lake kwa haraka na kununua gari la umeme la kampuni nyingine. Alipoenda kwa dalali wa magari ya mtumba, aligundua kuwa siku hiyo hiyo wateja wengine wawili walikuwa wamerudisha magari yao ya Tesla kwa sababu kama yake.
Katika mitandao ya kijamii ya wamiliki wa Tesla nchini Australia, kumekuwa na ripoti kadhaa za madereva wakidhihakiwa barabarani kwa kuendesha Tesla. Mtu mmoja alisimulia jinsi dereva mwingine alivyomfanyia ishara ya “L” kwa kidole kwenye paji la uso wake, ishara inayomaanisha "mshindwa" (loser).
Mbali na utata wa salamu ya Nazi, Musk ameendelea kuzua mgawanyiko barani Ulaya kwa kuonyesha waziwazi uungaji mkono wake kwa vyama vya siasa za mrengo wa kulia, kama vile chama cha Alternative für Deutschland (AfD) cha Ujerumani. Hali hii imepelekea anguko kubwa la mauzo ya Tesla barani Ulaya, ambapo mnamo Januari, mauzo yalishuka kwa asilimia 45. Nchini Ujerumani, Tesla ilishuhudia kushuka kwa asilimia 60 mnamo Januari na asilimia 76 mnamo Februari.
Pamoja na ushindani mkali kutoka kwa kampuni kama BYD ya China, inazidi kuwa wazi kuwa tabia ya Musk inachangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mvuto wa Tesla katika masoko mengi.
Hali hii inaonyesha jinsi ambavyo msimamo wa kiongozi wa kampuni unaweza kuathiri moja kwa moja mauzo na sifa ya bidhaa. Watumiaji wengi wanaonekana kuwa tayari kubadilisha bidhaa wanazotumia ikiwa wanaona kuwa maadili ya kiongozi wa kampuni hayalingani na maadili yao.
Hivyo, Tesla inakabiliwa na changamoto kubwa ya kujenga upya sifa yake na kuwarejesha wateja ambao wamepoteza imani kutokana na matendo ya Elon Musk.