Serikali ya Uingereza imetoa wito kwa raia wake kuepuka safari zisizo za lazima kuelekea baadhi ya maeneo ya Thailand na Kambodia, kufuatia mapigano makali yaliyozuka kwa mara ya kwanza baada ya miaka 13. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imewataka wananchi wake kujiepusha na maeneo hatarishi, hasa yale yaliyo ndani ya kilomita 50 kutoka mpaka wa Thailand na mikoa ya Oddar Meanchey na Preah Vihear huko Kaskazini mwa Kambodia.
Maeneo haya yamebainishwa kuwa na hatari kubwa kutokana na mashambulizi ya risasi, mapigano ya ana kwa ana, na uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini ambayo hayajalipuka. Hali hii imesababisha baadhi ya maeneo ya utalii kufungwa kando ya mpaka huo, na hivyo kuathiri shughuli za kawaida za kijamii na kiuchumi. Mapigano haya yalianza baada ya nchi jirani za Kusini Mashariki mwa Asia, Thailand na Kambodia, kugombana kuhusu mzozo wa mpaka wao.
Mapigano hayo yaliripotiwa kutokea katika maeneo sita tofauti ya mpaka, huku yakihusisha matumizi ya silaha nzito zikiwemo roketi za BM-21. Katika mapigano hayo, watu kumi na wawili walipoteza maisha, wakiwemo raia kumi na mmoja na mwanajeshi mmoja. Kufuatia ghasia hizo za asubuhi, nchi zote mbili zilianza kulalamikiana, zikilaumiana kwa kuanzisha mapigano hayo. Hali hii imepelekea uhusiano kati ya Thailand na Kambodia kudorora kwa kiwango kikubwa, na sasa unatajwa kuwa mbaya zaidi katika miongo kadhaa.
Mzozo huu wa mpaka umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu, ukihusisha eneo la hekalu la kale la Preah Vihear ambalo limetambuliwa kama urithi wa dunia na UNESCO. Ingawa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitoa uamuzi mwaka 1962 kuwa hekalu hilo ni mali ya Kambodia, eneo linalolizunguka limeendelea kuwa chanzo cha mvutano na mapigano ya mara kwa mara. Raia wa Tanzania wanaopanga safari za kimataifa wanashauriwa kufuatilia miongozo ya usafiri kutoka nchi wanazopanga kuzitembelea na pia kuzingatia ushauri wa ubalozi wa Tanzania katika nchi husika.