Rais wa Marekani, Donald Trump, amepongeza matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bunge la Shirikisho la Ujerumani (Bundestag), akisema kuwa ushindi wa chama cha kihafidhina ni "siku kubwa kwa Ujerumani na Marekani."
Trump alitoa kauli hiyo kupitia mtandao wake wa kijamii, akieleza kuwa "chama cha kihafidhina kinaonekana kushinda uchaguzi huu mkubwa na uliotarajiwa kwa hamu." Alisema kuwa, kama ilivyo kwa Marekani, Wajerumani wamechoshwa na sera zisizo na mantiki kuhusu nishati na uhamiaji, na alieleza matumaini yake kwamba vyama vya kihafidhina vitaendelea kushinda chaguzi zaidi siku zijazo.
Ujerumani ilifanya uchaguzi wake wa Bunge la Shirikisho mnamo tarehe 23 Februari, huku matokeo ya awali yakionyesha kwamba muungano wa vyama vya kihafidhina, Christian Democratic Union (CDU) na Christian Social Union (CSU), umepata asilimia 29 ya kura na kinatarajiwa kuwa chama kikubwa zaidi bungeni. Chama cha mrengo mkali wa kulia, Alternative for Germany (AfD), kilipata asilimia 19.5, huku chama cha Kansela Olaf Scholz, Social Democratic Party (SPD), kikishika nafasi ya tatu kwa asilimia 16.
Awali, bilionea Elon Musk, ambaye anafahamika kuwa mshirika wa karibu wa Trump, alionyesha wazi uungaji mkono wake kwa chama cha AfD. Mnamo Januari, Musk alishiriki mkutano wa kampeni ya chama hicho kwa njia ya video, hatua iliyotafsiriwa kama msaada wake kwa chama hicho cha mrengo mkali wa kulia.