Katika hali inayoonekana kama mkakati mpya wa kidiplomasia na shinikizo la kijeshi, Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa kauli nzito kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Ameashiria uwezekano wa Marekani kuipelekea Ukraine makombora ya masafa marefu aina ya 'Tomahawk' iwapo mzozo huo hautapata suluhu ya haraka, huku akisisitiza umuhimu wa mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump alibainisha kuwa ombi la msaada wa makombora hayo limetoka kwa Ukraine. Alisema, "Inawezekana ikabidi niseme, 'Tazameni: kama vita hivi havitatatuliwa, nitawapelekea (Ukraine) makombora ya Tomahawk.'" Hata hivyo, aliongeza kwa haraka kuwa ana matumaini makubwa ya vita kumalizika kwa amani na kwamba Urusi haitahitaji kuona silaha hizo zikiingia katika eneo la mzozo. Kauli hii inatafsiriwa kama njia ya kuweka shinikizo mezani, ambapo chaguo la kwanza ni mazungumzo ya amani, lakini ikiwa yatakwama, msaada wa kijeshi wa hali ya juu utafuata.
Msimamo huu wa Trump umekuja huku Urusi ikiwa tayari imeonyesha upinzani mkali dhidi ya wazo lolote la Marekani kuihusha Ukraine na silaha za masafa marefu. Rais Vladimir Putin, alikuwa ametoa onyo kali mapema mwezi huu akisema kitendo hicho kitasababisha "uharibifu wa mahusiano kwa kiwango kipya kabisa, cha ubora tofauti" kati ya Moscow na Washington.
Vilevile, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, alisisitiza kauli hiyo akionya kwamba uhusiano baina ya mataifa hayo mawili utaingia kwenye "mzingo wa uhasama mkali." Onyo hili kutoka kwa viongozi waandamizi wa Urusi linaonesha ni kwa kiasi gani wanaona hatua hiyo kama uchokozi wa moja kwa moja unaoweza kupanua wigo wa vita na kuongeza hatari ya makabiliano makubwa zaidi.