Urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Angola, ulioasisiwa tangu enzi za ukombozi wa Kusini mwa Afrika, umeingia katika awamu mpya baada ya Balozi Mteule wa Angola nchini, Domingos de Almeida da Silva Coelho, kuwasilisha rasmi nakala za hati zake za utambulisho. Hati hizo zilipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, Balozi Kombo alimkaribisha mwakilishi huyo mpya na kumhakikishia ushirikiano kamili kutoka kwa serikali ya Tanzania. Alikumbusha kuwa uhusiano wa kindugu baina ya nchi hizi mbili ulianza tangu Angola ilipopata uhuru wake mwaka 1975 na umekuwa imara tangu wakati huo.
Waziri Kombo alieleza kuwa ushirikiano huo umezaa matunda katika nyanja nyingi, ikiwemo biashara, uwekezaji, na kubadilishana utaalamu katika sekta za kimkakati kama mafuta na gesi, madini, na ulinzi. Vilevile, alitaja maeneo mengine muhimu ya ushirikiano kama vile afya, utalii, ufugaji wa samaki, usafiri wa majini, miundombinu ya reli, na Uchumi wa Bluu.
Kwa upande wake, Balozi Mteule Domingos de Almeida da Silva Coelho aliipongeza Tanzania kwa kudumisha uhusiano huu wa kindugu. Aliahidi kuwa katika kipindi chake cha uwakilishi, atafanya kazi kwa bidii sio tu kuendeleza yaliyopo, bali pia kutafuta fursa mpya za ushirikiano zitakazonufaisha pande zote mbili na kuimarisha zaidi uhusiano wa Kusini-Kusini.