Ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Ufalme wa Uholanzi umeanza ukurasa mpya kufuatia Balozi Mteule wa nchi hiyo, Marjo Johanna Jacoba Crompvoets, kuwasilisha rasmi Nakala za Hati zake za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Waziri Kombo alimkaribisha rasmi Balozi Crompvoets na kumpongeza kwa uteuzi wake, huku akimhakikishia ushirikiano usioyumba kutoka kwa Serikali ya Tanzania katika kipindi chake chote cha utumishi nchini.
Balozi Kombo alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Uholanzi kwa kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa Tanzania. Alitaja miradi mingi inayofadhiliwa na Uholanzi ambayo imegusa moja kwa moja maisha ya wananchi katika sekta muhimu kama vile miundombinu, afya, elimu, biashara, utalii na uwekezaji.
Kwa upande wake, Balozi Crompvoets aliishukuru Tanzania kwa ukarimu na ushirikiano thabiti uliopo. Aliahidi kuwa katika kipindi chake, ataendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano huo, akieleza kuwa Uholanzi itaweka mkazo maalum katika maeneo ya kipaumbele yatakayoleta matokeo ya haraka, hususan katika kuendeleza sekta ya kilimo cha kisasa cha mbogamboga, matunda na maua (horticulture), eneo ambalo Uholanzi ina utaalamu wa hali ya juu.