Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi, amepanga kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, hatua inayokuja wakati taifa hilo likikabiliwa na mzozo mkubwa wa waasi wa M23 katika maeneo ya mashariki.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa msemaji wa ofisi ya rais, Tshisekedi ameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na shinikizo la ndani kuhusu namna serikali yake inavyoshughulikia uvamizi wa waasi wa M23, ambao wanadaiwa kupata msaada kutoka Rwanda.
Mashariki mwa Congo imekuwa ikikumbwa na mapigano makali, huku waasi wa M23 wakidhibiti maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini. Hali hii imeongeza hofu ya kuzuka kwa vita vikubwa zaidi na kuibua mjadala mkali kutoka kwa wanasiasa wa upinzani, ambao wanatabiri kuwa utawala wa Tshisekedi unaweza kuyumba endapo hali itaendelea kuwa mbaya.
Akizungumza Jumamosi, Rais Tshisekedi alitoa wito wa mshikamano wa kitaifa ili kukabiliana na waasi. "Lazima tuungane... tusimame pamoja kukabiliana na adui," alisema.
Msemaji wa rais, Tina Salama, alithibitisha kuwa Tshisekedi atafanya mabadiliko katika uongozi wa serikali, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu muundo wa serikali hiyo mpya ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, hatua hiyo imepokelewa kwa mitazamo tofauti, huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakikosoa vikali mkakati huo. Herve Diakiese, mmoja wa wapinzani wakubwa wa serikali, alisema kuwa juhudi za Tshisekedi ni za kujihami kisiasa badala ya kutafuta suluhisho la kweli kwa taifa.
"Tshisekedi anajali zaidi kuokoa mamlaka yake, wakati sisi tunajali zaidi kuokoa Congo, jambo ambalo linaweza kufanikiwa chini yake au bila yeye," alisema Diakiese.
Wakosoaji wanasema kuwa mkakati wa kijeshi wa serikali dhidi ya waasi wa M23 haujaonyesha mafanikio makubwa, na hivyo kuibua maswali kuhusu ufanisi wa hatua zinazochukuliwa.
Matarajio sasa yanaelekezwa kwa Rais Tshisekedi kuona ikiwa serikali hii mpya ya umoja wa kitaifa itasaidia kurejesha utulivu mashariki mwa Congo na kupunguza mvutano wa kisiasa ndani ya nchi hiyo.