Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ameishutumu Ubelgiji kwa kuchochea mivutano kati ya Rwanda na mataifa mengine ya Afrika, akisisitiza kuwa nchi yake iko tayari kukabiliana na taifa hilo la Ulaya.
Akizungumza mjini Kigali, Rais Kagame alieleza kuwa Ubelgiji, ambayo ilikuwa mkoloni wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo), imekuwa ikihamasisha vikwazo dhidi ya Rwanda kwa miaka mingi.
"Ubelgiji imekuwa ikihusika katika mauaji ya raia wa Rwanda kwa muda mrefu. Wanarudi na kuondoka kila mara huku wakiendeleza njama zao. Tumewaonya kwa miaka mingi, na sasa tunawajulisha tena kuwa Rwanda haitanyamaza," alisema Kagame.
Rwanda imekuwa ikikabiliwa na ongezeko la vikwazo kutoka kwa mataifa makubwa duniani, yanayohusiana na tuhuma za kuisaidia kundi la waasi la M23 linalopigana katika eneo la Mashariki mwa DR Congo.
Rais Kagame aliwahakikishia wananchi wa Rwanda kuwa taifa hilo liko tayari kupambana na changamoto zinazotokana na vikwazo hivyo na kuendelea kulinda maslahi yake.
Mvutano kati ya Rwanda na Ubelgiji umeendelea kwa muda mrefu, ukionyesha changamoto kubwa katika diplomasia kati ya mataifa ya Afrika na waliokuwa wakoloni wao.