Mjane wa Rais wa kwanza wa Namibia, Sam Nujoma, Bi. Kovambo Nujoma, amemuelezea mumewe kama mtu mnyenyekevu na aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa nchi yake. Akizungumza kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake wakati wa Ibada ya Kitaifa ya Kumbukumbu ya mumewe katika Uwanja wa Uhuru, Windhoek, Ijumaa, Kovambo alieleza jinsi unyenyekevu wa Nujoma ulivyoonekana hata katika maisha yao ya nyumbani.
Akirejea safari yao ya maisha, Kovambo alisema walikutana katika miaka ya 1950 huko Walvis Bay, wakati ubaguzi wa rangi ulipokuwa umekithiri. Licha ya mazingira hayo magumu, upendo wao ulizidi vikwazo vya kikabila na kuwa kiungo thabiti cha mshikamano wao.
"Wetu ulikuwa upendo ulioimarika licha ya sheria za kikoloni zilizolenga kutugawanya. Tulifunga ndoa Mei 6, 1956, tukiunganishwa si tu na mapenzi yetu, bali pia na ndoto ya Namibia huru,” alisema.
Kovambo alisimulia changamoto walizokumbana nazo kama familia, hasa baada ya Nujoma kwenda uhamishoni. Alisema kuwa mara kwa mara walikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya usalama vya Afrika Kusini, lakini hata katika hali hiyo ngumu, upendo wa mumewe uliendelea kuwa nguzo yao kuu.
Alifichua kuwa hali ilivyokuwa mbaya zaidi, aliamua kumfuata mumewe nchini Zambia mwaka 1978. "Ulikuwa uamuzi mgumu, lakini wakati wa kukutana tena ulikuwa wa furaha kubwa. Tulihisi kwamba upendo wetu haukuweza kuvunjwa na vita au changamoto," alisema.
Kovambo alieleza furaha yake ya kushuhudia uhuru wa Namibia mnamo Machi 21, 1990, akiwa kando ya mumewe, ambaye ndoto yake kubwa ilikuwa kuona taifa lake likijitawala. "Ilikuwa ni siku ya kutimiza ndoto yake, maono aliyoyashikilia kwa miaka mingi ya kujitolea na mateso," alisema.
Akizungumzia maisha yao ya kifamilia, alisema licha ya majukumu yake makubwa kama kiongozi wa taifa, Nujoma alibaki kuwa mume mwenye upendo na baba aliyejali familia yake. "Alikuwa chanzo cha hekima, faraja, na msaada kwetu sote. Alikuwa mtu mwenye nidhamu, lakini pia mpole, mkarimu na mwenye kujali wengine," alisema.
Kwa kumalizia, Kovambo alitoa heshima zake kwa mume wake, akisema urithi wake utaendelea kuishi katika vizazi vijavyo. "Mume wangu mpendwa, utaendelea kuishi mioyoni mwetu. Urithi wako utabaki kuwa mwanga unaoongoza vizazi vijavyo. Pumzika kwa amani, mpenzi wangu," alisema.