Norway Kikaangoni: Shinikizo la Trump kwa Tuzo ya Nobel Lazua Hofu ya Vikwazo

international | Fri Oct 10 2025


Norway Kikaangoni: Shinikizo la Trump kwa Tuzo ya Nobel Lazua Hofu ya Vikwazo

Hali ya wasiwasi imetanda nchini Norway, saa chache kabla ya kutangazwa kwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel hapo kesho, Oktoba 10. Wasiwasi huo hautokani na nani atashinda, bali na "madhara ya baadae" endapo mshindi hatakuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye amekuwa akifanya kampeni kubwa na kuweka shinikizo ili tuzo hiyo iende kwake.


Vyanzo vya habari, vikiwemo shirika la Bloomberg, vinaripoti kuwa Norway inahofia uwezekano wa kukumbwa na vikwazo vya kiuchumi na kidiplomasia endapo jina la Trump halitatangazwa. Tayari, nchi hiyo ipo kwenye mazungumzo magumu ya kibiashara na Marekani kuhusu uwezekano wa kutozwa ushuru wa asilimia 15 kwa bidhaa zake. Hofu kubwa zaidi ipo kwenye Mfuko wake Mkuu wa Uwekezaji wa Taifa, wenye thamani ya Dola za Kimarekani trilioni 2 (takriban Shilingi za Kitanzania trilioni 5,000), ambao ni mfuko mkubwa zaidi duniani na asilimia 40 ya uwekezaji wake upo nchini Marekani.


Shinikizo kutoka kwa Trump na timu yake limekuwa wazi. Mtoto wake wa kiume, Eric Trump, aliandika kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) akiwataka watu warudufu ujumbe wake endapo wanaamini baba yake anastahili Tuzo ya Amani. Ikulu ya White House nayo ilichapisha picha ya Rais Trump akiongea na simu na kuandika "Rais wa Amani."


Trump mwenyewe, akizungumza na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Finland, Alexander Stubb, alisema, "Mimi ndiye mtu pekee katika historia kumaliza vita nane ndani ya miezi tisa. Sikufanya hivi ili nipate tuzo, nilifanya hivi kuokoa maisha ya watu wengi."


Hata hivyo, Kamati ya Nobel ya Norway imeweka msimamo wake wazi. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jørgen Watne Frydnes, ameliambia gazeti la Verdens Gang (VG) kwamba "mshindi wa mwaka huu alishaamuliwa tangu Oktoba 6," siku mbili kabla hata ya Trump kutangaza kusainiwa kwa makubaliano ya amani ya Gaza.


Zaidi ya hayo, katika mahojiano na shirika la utangazaji la umma (NRK), Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa makubaliano ya amani ya Mashariki ya Kati yatazingatiwa kwa ajili ya tuzo ya mwaka ujao, na si ya mwaka huu, kwani mchakato wa uteuzi wa mwaka huu ulifungwa Januari 31.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Espen Barth Eide, pia amesisitiza kuwa, "Serikali ya Norway haiingilii kwa vyovyote vile maamuzi ya Kamati ya Nobel." Kauli hii inaiweka Norway katika hali tete, ikijaribu kulinda uhuru wa kamati hiyo huku ikijiandaa kwa uwezekano wa hasira za kiongozi wa taifa lenye nguvu zaidi duniani.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.