Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanzisha mkakati maalum nchi nzima unaolenga kuwafikia na kuwasajili wananchi wote wenye ulemavu, ikisema hakuna mwananchi atakayeachwa nyuma katika kupata haki yake ya msingi ya utambulisho wa kitaifa. Hatua hii inalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ambapo kundi hili muhimu limekuwa likikumbana na vikwazo vya kufika katika ofisi za NIDA kutokana na hali zao maalum.
Akizungumza leo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Vitambulisho wa NIDA, Edison Guyai, alieleza kuwa zoezi hili ni sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), yanayoitaka kila nchi kuhakikisha kila raia anakuwa na utambulisho halali ifikapo mwaka 2030. Alisema NIDA inatambua kuwa watu wenye ulemavu wanahitaji huduma ya kipekee, hivyo wameamua kuwafuata walipo au kuwakusanya sehemu maalum ili kurahisisha usajili wao.
"Tunafahamu changamoto zao zinawazuia kuja ofisini kwetu, kwa hiyo tumeona ni wajibu wetu kuwatafutia utaratibu wa kuwahudumia kwa pamoja. Hii itatusaidia pia kusikiliza maoni yao ili tuendelee kuboresha mifumo yetu ya utoaji huduma kwao," alifafanua Guyai. Alisisitiza kuwa kitambulisho cha taifa ni muhimu kwa usalama wa nchi na upatikanaji wa huduma zote za kijamii na kiuchumi, kwani bila utambulisho, ni vigumu kwa mwananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Wakati huo huo, NIDA imetoa wito kwa umma kwa ujumla kuacha tabia ya kusubiri hadi dakika ya mwisho kutafuta vitambulisho. Guyai alibainisha kuwa ofisi zao mara nyingi huzidiwa na watu wengi wanaojitokeza pale tu wanapokwama kupata huduma fulani au wakati wanafunzi wanahitaji kwa ajili ya kujiunga na vyuo. Aliwashauri wananchi, hasa vijana wanaofikisha umri wa miaka 18, kujisajili mapema ili kuepuka usumbufu.
Aidha, Mamlaka imewakumbusha wananchi waliosajiliwa mwaka jana na bado hawajachukua vitambulisho vyao wafanye hivyo mara moja. Ilielezwa kuwa kuna idadi kubwa ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa na kuna hatari ya kufungiwa kwenye mfumo, jambo litakalowalazimu wamiliki kuanza upya mchakato. "Ili kuepuka usumbufu, tunawasihi wote wenye vitambulisho vyao NIDA wakavichukue kwa wakati," alisisitiza Guyai.