Mwandishi Maarufu wa Israel Aishutumu Nchi Yake kwa Mauaji ya Kimbari Gaza

international | Sat Aug 02 2025


Mwandishi Maarufu wa Israel Aishutumu Nchi Yake kwa Mauaji ya Kimbari Gaza

Mwandishi maarufu wa Israel, David Grossman, mshindi wa tuzo ya kifahari ya fasihi ya Man Booker, ametoa shutuma kali dhidi ya Serikali yake, akidai inatekeleza mauaji ya kimbari (genocide) huko Gaza. Katika mahojiano na gazeti la Italia la La Repubblica, Grossman alisema ameshindwa tena kuepuka kutumia neno hilo, akielezea mazingira ya sasa kama "genocide" kutokana na matukio yanayoendelea.


Kauli ya mwandishi huyo imekuja baada ya mashirika mawili makubwa ya kutetea haki za binadamu ndani ya Israel kutoa ripoti za wazi zinazoeleza kuwa nchi hiyo inafanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Grossman, ambaye familia yake iliathirika na mauaji ya kimbari ya Wanazi (Holocaust), alionyesha masikitiko makubwa na kushangazwa na jinsi nchi yake imeweza kufikia hatua hii. “Ninajiuliza, tulifika wapi? Ni vipi tunaweza kushtumiwa kwa mauaji ya kimbari?” alihoji.


Grossman alikiri kuwa alikuwa akipinga kutumia neno “genocide” kwa muda mrefu, lakini sasa hawezi tena kuliepuka. “Baada ya kusoma magazeti, kuona picha, na kuzungumza na watu waliokuwa huko, sioni njia nyingine,” alieleza. Alilinganisha mauaji ya kimbari na “theluji inayoteleza kutoka mlimani” (avalanche), akimaanisha kuwa mara inapoanza kutajwa, inakuwa kubwa zaidi na kuleta uharibifu na mateso makubwa.


Akizungumzia kiini cha matatizo haya, Grossman alidai kuwa “laana ya Israel” ilianza mwaka 1967 na uvamizi wake katika maeneo ya Palestina, akisema uvamizi huo uliwaathiri kimaadili. Mwandishi huyu, ambaye alishinda tuzo ya Man Booker mwaka 2017 kwa riwaya yake ya "A Horse Walks Into a Bar" na tuzo nyingine kubwa ya Israel mwaka 2018, amekuwa mkosoaji mkuu wa Serikali ya Benjamin Netanyahu.


Kuhusu suala la kutambuliwa kwa Serikali ya Palestina, Grossman alionesha kuunga mkono wazo hilo, akisema linaweza kuwa na faida zaidi kushughulika na Serikali halisi ya Palestina badala ya mamlaka isiyoeleweka. Hata hivyo, aliweka masharti, akisema inahitajika kuweka wazi sheria zinazokataza silaha na kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi ulio huru na wa uwazi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.