Hali ya wasiwasi inazidi kutanda katika Ukanda wa Gaza huku jeshi la Israel likijiandaa kuingia katikati ya Jiji la Gaza. Katikati ya mvutano huo, zimeibuka tuhuma nzito kutoka upande wa Israel kwamba kundi la Hamas linawazuia kimakusudi raia wa Kipalestina kukimbilia maeneo salama ya kusini, na hivyo kuwageuza kuwa "ngao za binadamu."
Shutuma hizi zinatokana na madai kuwa Hamas inatumia mbinu hiyo ili kupunguza kasi ya mashambulizi ya Israel na kuchafua sifa ya taifa hilo kimataifa kwa kusababisha vifo vingi vya raia. Jeshi la Israel limetoa ushahidi wa mazungumzo ya simu yaliyorekodiwa ambapo mkazi mmoja wa Gaza anasikika akimweleza afisa wa Israel, "Tunataka kuelekea kusini, lakini Hamas wanatuzuia." Mkazi huyo aliongeza kuwa wapiganaji wa Hamas wamefunga barabara kuu na kuwaambia watu "Hakuna pa kwenda, rudini makwenu."
Vyanzo vya habari kutoka Wizara ya Ulinzi ya Israel vinadai kuwa Hamas pia inaeneza propaganda za uongo, ikidai kuwa maeneo ya usalama yaliyotengwa kusini hayana mahema, chakula, wala huduma za matibabu. Zaidi ya hayo, Hamas inaripotiwa kutumia mbinu za vitisho, ikiwemo kuwapiga na kuwafyatulia risasi raia wanaojaribu kuondoka, huku ikiendesha kampeni ya kuwataka watu wasiondoke kwa kisingizio cha "wajibu wa kizalendo."
Chanzo kimoja cha usalama kililiambia gazeti la Jerusalem Post kwamba lengo la Hamas ni "kuwabakiza raia wengi iwezekanavyo Jiji la Gaza ili watumike kama ngao dhidi ya mashambulizi ya Israel." Lengo kuu, kulingana na chanzo hicho, ni kutumia vifo vya raia kama silaha ya kuishinikiza jamii ya kimataifa iingilie kati na kusitisha vita. "Hamas wanaona vifo vya raia kama nyenzo ya kimkakati ya kuharibu sifa ya Israel duniani," kilisema chanzo hicho. Inakadiriwa kuwa kati ya wakazi milioni moja wa Jiji la Gaza, ni watu kati ya 60,000 na 80,000 tu ndio wamefanikiwa kuhama tangu Israel ilipotoa onyo la kuondoka wiki mbili zilizopita.
Wakati hayo yakijiri, Hamas ilitoa taarifa ikisema iko tayari kwa "makubaliano ya kina" na Israel, lakini pendekezo hilo lilikataliwa vikali na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliyeliita "udanganyifu usio na jipya." Akichangia katika suala hilo, Rais wa Marekani, Donald Trump, aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii akisema, "Iambieni Hamas iwaachilie mateka 20 mara moja. Hilo likifanyika, hali itabadilika haraka. Vita vitaisha."