Muda mfupi tu baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kupuuza shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano na kutangaza kuendeleza vita mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, jeshi la nchi hiyo limefanya mashambulizi makali katika Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya makumi ya raia wasio na hatia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, mamlaka za afya za Gaza zimethibitisha kuwa takriban watu 59 wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya angani na milipuko ya risasi kutoka kwa wanajeshi wa Israel. Vifo hivi vimeongeza simanzi na taharuki katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu.
Maafa makubwa yameripotiwa katika kambi za wakimbizi. Katika shambulio moja la kinyama kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, familia nzima ya watu tisa iliuawa papo hapo wakiwa ndani ya nyumba yao. Saa chache baadaye, shambulio jingine katika kambi hiyo hiyo lilisababisha vifo vya watu wengine 15, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.
Ukanda wa kusini na kati mwa Gaza nao haukusalimika, ambapo raia sita waliokuwa wakisubiri kwa hamu msaada wa kibinadamu walipigwa risasi na kuuawa na wanajeshi wa Israel. Hali ya hofu imezidi kutanda hata katika maeneo ya hospitali; katika Hospitali ya Al-Helou iliyoko Gaza City, lango kuu lilifungwa baada ya ndege zisizo na rubani (drones) za Israel kuanza kuzunguka angani, na hivyo kuzua hofu kwa wagonjwa na wafanyakazi.
Mashambulizi haya ya kikatili yamefanyika mara tu baada ya hotuba ya Netanyahu kwenye Umoja wa Mataifa, ambapo alisisitiza kuwa "Hamas lazima imalizwe," akionyesha wazi dhamira ya Israel ya kuendeleza vita bila kujali wito wa jamii ya kimataifa.
Wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea, hali ya huduma za afya jijini Gaza inazidi kuwa mbaya kila kukicha. Tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi ya ardhini tarehe 15 mwezi huu, kliniki mbili zimeharibiwa kabisa na mashambulizi ya angani, hospitali mbili zimefungwa, na shirika la kimataifa la msaada wa kitabibu, Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), limelazimika kusitisha shughuli zake zote jijini Gaza.