Kumetokea kashfa na tukio la aibu kubwa katika eneo takatifu la Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro lililopo Mji wa Vatikani, ambalo ni kanisa kubwa zaidi ulimwenguni na makao makuu ya Kanisa Katoliki. Mwanamume mmoja amezua mshtuko mkubwa baada ya kunaswa akifanya kitendo cha kukojoa juu ya madhabahu kuu, mbele ya mamia ya watalii na mahujaji waliokuwa wamemiminika eneo hilo.
Tukio hili la kudhalilisha, lililotokea majira ya saa tatu na nusu asubuhi kwa saa za huko, liliwashtua wengi walioshuhudia mwanamume huyo akipanda kwenye madhabahu, akishusha suruali yake na kuanza kujisaidia bila hofu. Video za tukio hilo zilisambaa kwa kasi mitandaoni, zikionyesha walinzi wa kanisa wakimkimbilia kwa haraka na kumzuia kabla ya kumshusha chini kwa nguvu.
Msemaji Mkuu wa Vatikani, Matteo Bruni, alithibitisha kutokea kwa kisa hicho na kueleza kuwa mhusika ni mtu anayesumbuliwa na matatizo makubwa ya akili. "Baada ya kukamatwa na polisi wa Vatikani, mtu huyo amekabidhiwa kwa mamlaka za Italia kwa hatua zaidi," alisema Bwana Bruni katika taarifa yake kwa shirika la habari la Italia, ANSA.
Hata hivyo, hili si tukio la kwanza la aina yake kutokea kwenye madhabahu hiyo takatifu. Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya watu wenye tabia za ajabu wanaovamia eneo hilo. Mwezi Februari mwaka huu, mwanamume mwingine alipanda juu ya madhabahu na kuanza kurusha chini vinara sita vya mishumaa.
Kadhalika, mwaka 2023, mwanamume mmoja raia wa Poland alivua nguo zote karibu na madhabahu na kuandika mgongoni mwake ujumbe wa "Waokoeni watoto wa Ukraine" kama sehemu ya maandamano. Alikamatwa na askari wa Vatikani bila upinzani na kupigwa marufuku ya kuingia eneo hilo. Matukio haya yanaibua maswali kuhusu usalama wa maeneo matakatifu na yenye umuhimu wa kihistoria duniani.