Kundi lenye nguvu la wanamgambo nchini Lebanon, Hezbollah, linadaiwa kubuni mbinu mpya za kupitisha silaha na fedha kutoka Iran, kwa kulenga kutumia Bandari ya Beirut, baada ya njia yake ya jadi kupitia Syria kukatizwa. Taarifa hizi zimeripotiwa na chombo cha habari cha Saudia, Al Hadath, kikizitaja duru za Magharibi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya Magharibi, afisa mwandamizi wa usalama ndani ya Hezbollah, anayejulikana kama Wafiq Safa, anadaiwa kuwa katika harakati za kuchukua udhibiti wa idara ya forodha katika Bandari ya Beirut. Lengo kuu la mpango huu linatajwa kuwa ni kuwezesha uingizaji wa vifaa vya kijeshi na fedha kutoka Iran moja kwa moja kupitia baharini hadi Lebanon.
Inaarifiwa kuwa vitengo maalum vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC), hususan Kikosi cha Quds kupitia vitengo vyake vya 190 na 700 vinavyojihusisha na uratibu wa vifaa na usafirishaji haramu, vinapanga kusaidia Hezbollah katika mpango huu. Misaada hiyo inaweza kupitia njia za moja kwa moja hadi Lebanon au kupitia nchi za tatu kama njia mbadala.
Hata hivyo, duru hizo zimeonya kuwa hatua hii inaweza kuleta maafa mengine kama yale ya mlipuko mkubwa uliotokea katika Bandari ya Beirut mnamo Agosti 2020. Vyanzo hivyo vimetoa wito kwa serikali ya Lebanon kuchukua hatua za haraka kuzuia uwezekano huu. Bandari ya Beirut iliharibiwa vibaya tarehe 4 Agosti 2020, baada ya takriban tani 2,750 za kemikali ya ammonium nitrate, zilizokuwa zimehifadhiwa ghalani kwa miaka sita, kulipuka na kusababisha vifo vya watu 214 na uharibifu mkubwa. Ingawa bandari hiyo ilifungwa kwa muda, imekuwa ikifanyiwa ukarabati taratibu.
Jaribio hili la Hezbollah la kutumia njia ya bahari linakuja baada ya njia ya ardhini kutoka Iran kupitia Syria, ambayo ilikuwa ikitumiwa kwa muda mrefu, kukatizwa. Hii ilitokana na kuondolewa madarakani kwa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria mnamo Desemba mwaka jana (2024) kufuatia mashambulizi ya waasi. Utawala wa Assad ulikuwa na uhusiano wa karibu na Iran.
Hezbollah ilianzishwa mwaka 1982 kwa ufadhili wa Iran, awali ikiwa na lengo la kupambana na Israel iliyokuwa ikiivamia Lebanon wakati huo. Kundi hili limekuwa na nguvu kubwa kisiasa nchini Lebanon, likiwa na viti vingi bungeni, na pia lina nguvu kubwa kijeshi inayokaribia ya jeshi rasmi, huku likidhibiti kwa kiasi kikubwa eneo la Kusini mwa Lebanon.
Hata hivyo, kundi hilo limepata pigo katika miezi ya hivi karibuni. Wakati wa vita vya Gaza vilivyoanza Oktoba 2023, Israel ilifanya operesheni kali za kijeshi dhidi ya Hezbollah hadi kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano Novemba mwaka jana (2024), na kusababisha hasara kubwa kwa kundi hilo. Zaidi ya hayo, ushawishi wake wa ndani na nje ya nchi unadaiwa kupungua kufuatia kuchaguliwa kwa Rais Joseph Aoun mapema mwaka huu (2025), ambaye anaonekana kupendelewa zaidi na mataifa ya Magharibi.