Katika kile kinachoonekana kama moja ya ziara nzito na za kihistoria tangu ashike hatamu za kuliongoza Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV ametoa tamko ambalo limetikisa kuta za kidiplomasia duniani. Akiwa katika ziara yake ya kwanza kabisa nje ya Vatican, Kiongozi huyo amesisitiza bila kumung'unya maneno kuwa "Suluhisho la Mataifa Mawili" (Two-State Solution) ndiyo njia pekee na ya haki ya kumaliza uhasama wa muda mrefu na umwagaji damu kati ya Israel na Palestina.
Ujumbe Mzito Angani
Kauli hiyo imetolewa na Papa Leo XIV akiwa angani, akisafiri kutoka Uturuki kuelekea Lebanon, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kichungaji na kidiplomasia iliyoanza Novemba 27 na kutarajiwa tamati Desemba 2. Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake ya faragha na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, jijini Ankara, Papa alithibitisha kuwa walijadili kwa kina vita vinavyoendelea Gaza na Ukraine.
"Uturuki ina nafasi kubwa na muhimu sana katika kuleta amani kwenye migogoro hii," alisisitiza Papa, akionyesha imani yake kwa Ankara kama mpatanishi katika ukanda huo.
Msimamo wa Vatican vs Msimamo wa Israeli
Suala la Israel na Palestina limekuwa mwiba mchungu. Papa Leo XIV amerejea msimamo wa muda mrefu wa Vatican kwamba, ili haki itendeke, lazima kuwepo na taifa huru la Palestina (linalojumuisha Ukingo wa Magharibi, Gaza, na Jerusalem Mashariki) linaloishi bega kwa bega na Israel.
"Tunafahamu fika kuwa kwa sasa Israel haikubaliani na suluhisho hili," alisema Papa kwa masikitiko, "Lakini ninaamini hii ndiyo njia pekee ya kuleta haki kwa pande zote mbili. Sisi ni marafiki wa Israel pia, na tunajitahidi kuwa sauti ya kati ili kuwafikisha kwenye meza ya suluhu."
Kauli hii inakuja wakati ambapo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekuwa na msimamo mkali kama mwamba. Netanyahu amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema kuwa kuruhusu taifa la Palestina ni sawa na kuwapa "zawadi" kundi la Hamas, na kwamba hatayumbishwa na shinikizo lolote la kimataifa, iwe ni la mitandaoni au la viongozi wa dunia.
Kutua Kwenye Ardhi ya Mierezi: Lebanon
Baada ya Uturuki, ndege ya Papa imetua jijini Beirut, Lebanon. Hii ni nchi yenye historia ya kipekee Mashariki ya Kati, ikiwa na mchanganyiko mkubwa wa kidini ambapo takriban asilimia 30 ya watu ni Wakristo, huku wengine wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni.
Ulinzi umeimarishwa vilivyo. Magari ya msafara wa Papa yamepangwa kupita katika maeneo ya Kusini mwa Beirut, ambayo ni ngome kuu ya kundi la Hezbollah na ambayo imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya anga ya Israel mwaka jana. Licha ya hatari hiyo, viongozi wa dini zote wamempokea kwa mikono miwili. Sheikh Sami Abi Al-Muna, kiongozi mkuu wa madhehebu ya Druze, amesema, "Lebanon inahitaji mwanga wa matumaini, na ziara hii ndiyo huo mwanga."
Makovu ya Bandari ya Beirut
Ratiba ya Papa nchini humo imejaa hisia nzito. Amepanga kufanya maombi maalum katika eneo la Bandari ya Beirut, mahali ambapo mlipuko mkubwa wa mwaka 2020 ulitokea na kuua watu 218 huku ukiacha maelfu wakiwa wamejeruhiwa. Tukio hilo bado ni kidonda mbichi kwa Walebanon wengi.
Pia, atatembelea hospitali ya wagonjwa wa akili, moja ya vituo adimu nchini humo, kuonyesha ukaribu wake na wanaoteseka kisaikolojia kutokana na vita na hali ngumu ya maisha. Hata hivyo, kutokana na hali ya usalama, Papa hataenda Kusini mwa Lebanon ambako mapigano bado ni makali, ingawa kundi la Hezbollah limemtaka atumie sauti yake kukemea kile walichokiita "uonevu na uvamizi."
Ziara hii ya Papa Leo XIV ni kielelezo tosha kuwa Vatican haijakata tamaa na amani ya Mashariki ya Kati, ikiamini kuwa hata kwenye giza nene, upatanisho bado unawezekana.