Marekani na Urusi zimefanya mazungumzo ya marathoni yaliyodumu kwa saa 12 kujadili uwezekano wa kusitisha mapigano katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi TASS, mazungumzo hayo yalifanyika kwa faragha mnamo Machi 24 katika hoteli ya Ritz-Carlton huko Riyadh, Saudi Arabia. Mazungumzo hayo yalianza saa 4:00 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na kumalizika saa 4:30 usiku, yakijumuisha mapumziko mara tatu. Inatarajiwa kuwa taarifa ya pamoja itatolewa leo, Machi 25.
Marekani iliwakilishwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House, Mike Waltz, Mjumbe Maalum wa Ukraine na Urusi, Keith Kellogg, na Mkurugenzi wa Mipango ya Sera wa Wizara ya Mambo ya Nje, Michael Anton. Upande wa Urusi uliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Baraza la Shirikisho, Grigory Karasin, na Mshauri wa Mkurugenzi wa Shirika la Usalama la Shirikisho (FSB), Sergei Beseda.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema kuwa timu yao ya mazungumzo haikutoa maelezo ya kina kuhusu mazungumzo hayo walipoondoka kwenye ukumbi, lakini ilisema "makubaliano yamefikiwa."
Inaaminika kuwa mazungumzo hayo yalihusu zaidi usalama wa bahari ya Black Sea na uwezekano wa kufufua mpango wa usafirishaji wa nafaka kupitia bahari hiyo, unaojulikana kama 'Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi'.