Mapenzi Yaua Akili: Bosi wa FBI Atuma Makomandoo wa SWAT Kulinda 'Bebi' Wake, Ndege za Serikali Zageuka Daladala

international | Tue Nov 25 2025


Mapenzi Yaua Akili: Bosi wa FBI Atuma Makomandoo wa SWAT Kulinda 'Bebi' Wake, Ndege za Serikali Zageuka Daladala

Waswahili husema, "Mapenzi kikohozi, kuificha hauwezi," lakini inapofikia hatua ya kiongozi mkuu wa usalama kutumia rasilimali za taifa kufurahisha moyo wa mpenzi wake, hapo ndipo tunaposema, "Mapenzi yamezidi unga." Huko nchini Marekani, Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la FBI, Bwana Kash Patel, amejikuta katikati ya kashfa nzito inayohusisha matumizi mabaya ya ofisi, yote hayo ikiwa ni katika harakati za kumlinda na kumfurahisha mpenzi wake, mwimbaji nyota wa muziki wa Country, Alexis Wilkins.


SWAT Kulinda Mpenzi? Hii Mpya! Dunia inafahamu kuwa kikosi cha SWAT (Special Weapons and Tactics) ni "Wajeda" maalum waliofunzwa kukabiliana na magaidi, watekaji nyara, na wahalifu sugu wenye silaha nzito. Hawa si walinzi wa kwenye matamasha ya muziki. Lakini kwa Bwana Patel (45), hadhi ya mpenzi wake Bi. Wilkins (47) ilistahili ulinzi wa hadhi ya Rais.


Habari kutoka New York Times zimefichua kuwa katika tukio la kustaajabisha lililotokea majira ya mchipuko huko Atlanta, Patel aliwaagiza makomandoo wawili wa SWAT kwenda kutoa ulinzi kwa mpenzi wake alipokuwa akiimba kwenye mkutano wa Chama cha Wamiliki wa Bunduki (NRA).


Kichekesho ni kwamba, makomandoo hao walipofika na kufanya tathmini ya kiusalama, waligundua hakuna tishio lolote kwa mwanadada huyo na kuamua kuondoka zao. Kitendo hicho kilimuudhi Bwana Patel ambaye alimwashia moto kamanda wa kikosi hicho, akilalamika kwa uchungu, "Mmemwacha mpenzi wangu bila ulinzi!" Kana kwamba hiyo haitoshi, alikosoa kwanini hawakumpa ripoti ya kila hatua aliyopiga mpenzi wake, utadhani ni operesheni ya kijeshi vitani.


Ndege za Serikali Kama Bodaboda Ukiacha sarakasi za SWAT, maisha ya Bwana Patel yanaonekana kuwa ya "kula kuku kwa mrija" kwa kutumia kodi za wananchi. Imebainika kuwa mwezi Agosti, alitumia ndege ya serikali kwenda nchini Scotland kwa ajili ya safari binafsi ya kucheza Gofu na marafiki zake.

Wadadisi wa mambo wanasema kiongozi huyo amegeuza ndege za serikali (zikiwemo jeti ndogo na ndege kubwa) kuwa usafiri wake binafsi wa kumtembelea mpenzi wake kila anapojisikia. Huku akivuta sigara kubwa (cigars) na kutengeneza sarafu za ukumbusho kwa pesa ya umma, Patel anaonekana kuishi maisha ya kifalme ndani ya serikali.


'Wana wa Nchi' Wamjia Juu Tabia hii imewaudhi hata washirika wake wa karibu wa mrengo wa kisiasa wa MAGA (Make America Great Again). Grace Chong, ambaye ni mshawishi mkubwa wa kisiasa na mshirika wa karibu wa Steve Bannon (mpambe wa zamani wa Trump), hakuuma maneno. Kupitia mtandao wa X, alihoji kwa hasira:

"Hivi huyu Wilkins ni mkeo wa ndoa? Kama sivyo, kwanini walipa kodi wa Marekani wamgharamie ulinzi wa SWAT? Sisi inatuhusu nini?"


Uongozi au Ulimbukeni? Wataalamu wa masuala ya usalama wanatafsiri hii kama dalili ya "ulevi wa madaraka." Christopher O'Leary, ambaye ni kigogo wa zamani wa kitengo cha ugaidi cha FBI, amesema wazi kuwa kitendo cha kutumia makomandoo kwa ajili ya "bebi" na ndege za serikali kwa ajili ya Gofu ni uthibitisho wa kiongozi asiye na busara, asiyejua mipaka ya kazi yake, na mwenye kiburi cha madaraka.


Sakata hili linatoa funzo kwetu sote: Cheo ni dhamana, na mapenzi yasichanganywe na rasilimali za umma. Marekani sasa inawaka moto, huku wananchi wakihoji kama FBI imegeuka kuwa kampuni binafsi ya ulinzi (Private Security) kwa wapenzi wa vigogo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.