Hali ya kisiasa imekuwa tete katika taifa la kisiwani la Madagascar, baada ya Rais Andry Rajoelina kuchukua hatua ya dharura ya kuvunja baraza zima la mawaziri, kufuatia maandamano makubwa yanayoendeshwa na vijana nchi nzima. Vijana hao wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha, ikiwemo umasikini uliokithiri, na huduma duni za jamii kama vile kukatika mara kwa mara kwa umeme na maji.
Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni ya serikali usiku wa Jumatatu, Rais Rajoelina alitangaza kumfuta kazi Waziri Mkuu, Christian Ntsay, pamoja na mawaziri wengine wote. "Ikiwa watendaji serikalini wameshindwa kutimiza wajibu wao, tunakiri na tunaomba radhi," alisema Rais, huku akiahidi kutoa msaada kwa biashara zilizoathiriwa na ghasia na kueleza nia yake ya kufungua milango ya mazungumzo na vijana.
Hatua hii ya Rais imekuja baada ya maandamano mapya kuzuka tena siku ya Jumatatu. Awali, kufuatia maandamano ya Septemba 25 na 26 katika mji mkuu Antananarivo na miji mingine, Rais alimfuta kazi Waziri wa Nishati pekee, hatua ambayo haikuwaridhisha waandamanaji. Licha ya serikali kuvunjwa, vuguvugu la vijana la 'Z-Generation Movement' limeendelea kuitisha maandamano zaidi.
Hata hivyo, maandamano hayo yamekumbwa na ghasia. Umoja wa Mataifa (UN) uliripoti Jumanne kuwa takriban watu 22 walipoteza maisha na zaidi ya 100 kujeruhiwa wakati polisi walipojaribu kuyazima kwa nguvu maandamano ya wiki iliyopita. Serikali ya Madagascar imekanusha vikali takwimu hizo, ikisema zinatokana na uvumi. Kutokana na uporaji na uchomaji mali uliofuata, serikali imeweka amri ya kutotembea usiku katika mji mkuu.
Madagascar, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960. Kulingana na Benki ya Dunia, kufikia mwaka 2022, takriban asilimia 75 ya idadi ya watu nchini humo walikuwa wakiishi chini ya mstari wa umaskini, na kuifanya kuwa moja ya nchi maskini zaidi duniani.