MACHOZI YA GAZA: Umoja wa Mataifa wasema itagharimu Shilingi Trilioni 190 kuifuta ‘Jehanamu hii ya Duniani’, uchumi wafa kifo cha mende

international | Wed Nov 26 2025


MACHOZI YA GAZA: Umoja wa Mataifa wasema itagharimu Shilingi Trilioni 190 kuifuta ‘Jehanamu hii ya Duniani’, uchumi wafa kifo cha mende

Dunia imepigwa na butwaa baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kutoa ripoti nzito inayoelezea uharibifu uliotokana na vita vya Gaza, ukifananisha hali hiyo na "shimo la giza lililochimbwa na wanadamu wenyewe." Ripoti hiyo ya kusikitisha inabainisha kuwa itagharimu kiasi cha fedha kisichopungua Dola za Marekani bilioni 70 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 190) ili kuweza kuirudisha Gaza katika hali yake ya kawaida. Hii ni fedha nyingi mno ambayo inaweza kuendesha bajeti ya serikali ya Tanzania kwa miaka kadhaa mfululizo.


Uchumi Wasambaratika, Maendeleo Yafutika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD), katika ripoti yake iliyotolewa tarehe 25, limeeleza kuwa miaka miwili ya operesheni za kijeshi imeteketeza miundombinu, viwanda, na huduma za jamii kwa kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa. "Maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana kwa tabu kwa muda wa miaka 22, yamefutwa kabisa ndani ya miezi 15 tu," inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.


Takwimu zinaogopesha; kuanzia Novemba 2023 hadi Aprili mwaka huu, zaidi ya majengo 174,500 yameharibiwa vibaya. Hii ni sawa na asilimia 70 ya majengo yote ya Gaza. Pikiria mji kama Dar es Salaam, kisha asilimia 70 ya nyumba zote za Kariakoo, Magomeni, na Posta zigeuke vifusi; hiyo ndiyo hali halisi ya Gaza hivi sasa.


Umaskini wa Kutupwa

Kiuchumi, Gaza imerudi nyuma kiasi cha kutisha. Pato la Taifa (GDP) la maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu limeporomoka hadi kufikia viwango vya mwaka 2010. Lakini ukiiangalia Gaza pekee, hali ni mbaya zaidi.


Mwaka 2005, wastani wa pato la mtu mmoja Gaza lilikua Dola 2,508. Kabla ya vita mwaka 2022, lilishuka hadi Dola 1,253 kutokana na vikwazo. Lakini kufuatia vita vilivyoanza 2023, pato hilo liliporomoka hadi Dola 970 na mwaka huu wa 2024 limefikia kiasi cha aibu cha Dola 161 (Sawa na TZS 430,000 hivi kwa mwaka). Hii ina maana kuwa wakazi milioni 2.3 wa Gaza wameingia katika lindi la umaskini uliokithiri, wakikosa mahitaji yote ya msingi. Hata Ukingo wa Magharibi (West Bank) nao hausalimiki, ukikabiliwa na ongezeko la vurugu na vikwazo vya kutembea.


Amani ya Mashaka

Vita hivi, vilivyoanza Oktoba 7, 2023 baada ya shambulio la Hamas lililoua Waisraeli 1,200, vimesababisha vifo vya Wapalestina takriban 69,000, wengi wao wakiwa ni raia wasio na hatia. Ingawa makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa Oktoba 10 mwaka huu kwa upatanishi wa Marekani, hali bado ni 'shwari ya mpito'.


Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti kuwa tangu kuanza kwa makubaliano hayo ya amani, Wapalestina 342 wameuawa katika mashambulizi ya hapa na pale. Upande wa Israel nao umepoteza wanajeshi watatu. Hata hivyo, kuna mwanga kidogo wa matumaini huku kundi la Hamas na washirika wake wa Islamic Jihad wakijiandaa kukabidhi miili ya mateka wa Israel kama sehemu ya makubaliano hayo, ingawa Israel inalamika kuwa zoezi hilo linasuasua kinyume na makubaliano.


Swali linalobaki vichwani mwa wengi ni je, dunia itasimama pamoja kuisaidia Gaza kuinuka kutoka katika hili "shimo la mauti", au itabaki kuwa historia ya kidonda kisichopona?

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.