Serikali ya Lesotho imeonesha kuvutiwa sana na hatua kubwa ambazo Serikali ya Tanzania imepiga kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kusambaza nishati safi kwa maeneo ya vijijini. Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Lesotho, Tankiso Phapano, alieleza hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wataalamu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) akiwa ameambatana na ujumbe wa wataalamu wa sekta ya nishati kutoka nchini kwake.
"Tumekuwa tukifuatilia kwa karibu sana suala la nishati, na Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa na zimefanikiwa kwa upana wake. Tuko hapa leo hii kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza siri ya mafanikio ambayo imewafikisha hapa," alisema Bwana Phapano.
Alisifu juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi, akisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi nchini Tanzania.
Akizungumzia hali ya usambazaji wa nishati katika maeneo ya vijijini nchini Lesotho, Meneja wa Kitengo cha Umeme Vijijini (REU), Leloko Mokhutsoane, alisema kuwa kwa sasa shughuli hizo zinasimamiwa na kitengo ndani ya Shirika la Umeme la Lesotho (LEC). Hata hivyo, alieleza kuwa kutokana na kusuasua kwa ufanisi wa kitengo hicho na mahitaji makubwa ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya vijijini, nchi hiyo inapanga kuanzisha Wakala wake wa Nishati Vijijini.
"Hiki ni kitengo tu ndani ya shirika la umeme, na kinashughulika na umeme pekee, siyo nishati kwa upana wake. Kwa sasa, nasi tunataka kuwa na Wakala wa Nishati Vijijini kama ilivyo Tanzania ili suala la nishati safi liweze kujumuishwa na tusibaki tukifikiria umeme pekee," alisema Bwana Mokhutsoane.
Akielezea uendeshaji wa shughuli za REA nchini Tanzania kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wake, Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu, alisema kuwa wakati wakala huo ulipoanzishwa mwaka 2007, ni vijiji 506 pekee kati ya vijiji 12,318 vilivyokuwa vimefikiwa na umeme nchini.
Bwana Olotu alifafanua kuwa katika Tanzania Bara kuna vitongoji 64,359, na kati ya hivyo, vitongoji 33,657, sawa na asilimia 52.3, tayari vimefikishiwa umeme. Aliongeza kuwa kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji vingine 30,702 inaendelea vizuri, ambapo vitongoji 7,736 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi wa miradi, na REA iko katika hatua ya mwisho ya ununuzi wa wakandarasi kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji vingine 9,000, na mchakato huo unatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Ziara hii ya wataalamu kutoka Lesotho inaashiria nia yao ya dhati ya kujifunza kutokana na uzoefu wa Tanzania katika kusambaza nishati vijijini, ambayo inaweza kuwa mfano bora kwa nchi nyingine za Afrika zinazopambana na changamoto kama hizo.