Serikali Yatoa Ruzuku Kubwa kwa Mitungi ya Gesi Vijijini Kuhimiza Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia

economy | Fri May 23 2025


Serikali Yatoa Ruzuku Kubwa kwa Mitungi ya Gesi Vijijini Kuhimiza Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa Serikali imetoa ruzuku ya kati ya asilimia 20 hadi 50 kwa takribani mitungi 452,445 ya gesi ya LPG kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia nchini.


Akijibu maswali mbalimbali bungeni jijini Dodoma leo, Mei 23, 2025, Naibu Waziri Kapinga alieleza kuwa hatua hii inalenga kuwawezesha wananchi, hasa wale waishio vijijini, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yana madhara kwa afya na mazingira.


Kapinga alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega, aliyetaka kujua mkakati wa muda mfupi wa Serikali kuhakikisha wananchi wa vijijini wanatumia nishati safi ya kupikia. “Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pia itasambaza majiko banifu 200,000 kwa bei iliyopunguzwa hadi asilimia 75, pamoja na kuwezesha ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma zinazohudumia watu zaidi ya 100,” alisema Kapinga.


Aidha, alifahamisha kuwa Serikali imekamilisha kazi ya kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini, na sasa inaendelea kuhamasisha matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia umeme kama njia mojawapo ya kuendeleza matumizi ya nishati safi kwa wananchi wa vijijini.


Kapinga alibainisha kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka kumi, lakini Serikali ina mkakati wa matumizi bora ya nishati unaoshirikisha pia sekta binafsi katika kusaidia uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Akijibu swali la Mbunge wa Mbulu, Zacharia Isaay, kuhusu mikakati ya Serikali kuhakikisha vitongoji vyote vilivyokusudiwa kuunganishwa na umeme katika mwaka huu wa bajeti vinafikiwa katika muda uliobaki, Kapinga alisema Serikali ina mikakati na miradi mbalimbali ya kupeleka umeme vijijini. Alitaja mojawapo ya mikakati hiyo kuwa ni kupeleka umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo. Pia, Serikali imeanzisha mkakati wa kupeleka umeme katika vitongoji 20,000, ambapo awamu ya kwanza inahusisha kupeleka umeme katika vitongoji 9,000, na hatua iliyopo sasa ni kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kazi hiyo.


Kuhusu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest, aliyeuliza lini bei ya ruzuku ya Serikali imeanza kutumika kutokana na mitungi ya gesi kuendelea kuuzwa kwa bei ya juu, Kapinga alieleza kuwa kwa maeneo ya mjini, Serikali imetoa ruzuku hadi asilimia 25, na kwa maeneo ya vijijini ruzuku ni kati ya asilimia 50 hadi 75. Alitoa mfano kuwa mtungi uliokuwa unauzwa kwa Shilingi 45,000 kwa bei ya ruzuku unapatikana kwa kati ya Shilingi 17,000 hadi 21,000, akisema kuwa hii ni zaidi ya nusu ya bei ya awali. Aliongeza kuwa katika kila wilaya kuna takribani mitungi 3,255 inayopatikana kwa ruzuku, na akasisitiza kuwa mkakati huu ndio kwanza umeanza.


Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Yustina Rahhi, kuhusu mpango wa Serikali kuwapelekea jamii ya wafugaji teknolojia ya biogas au kuwajengea majiko yanayotumia samadi ya gesi, Kapinga alisema Serikali inatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (kupitia mfuko wa UNCDF), ambao unahusisha teknolojia alizozitaja mbunge.


Kuhusu swali la Mbunge wa Nyang’wale, Hussein Amar, kuhusu mpango wa Serikali kupeleka nishati safi ya kupikia katika shule za sekondari 19 za mchana na 12 za bweni zilizopo wilayani Nyang’wale kwa ajili ya kulinda mazingira, Kapinga alisema Wizara ya Nishati ina mpango wa kupeleka nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Katika hatua nyingine, Kapinga alizishauri Halmashauri zote nchini kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika taasisi zilizopo kwenye maeneo yao kwa kutumia mapato ya ndani.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.