Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeweka malengo ya kukamilisha upelekaji wa umeme katika vitongoji 16,500 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Hii inafuatia kuwekwa kwa mifumo maalum ya kusimamia wakandarasi waliosaini mikataba ili kuhakikisha wanawajibika katika utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ndani ya muda uliopangwa.
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa pili na kikao cha sita cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huo mkoani Morogoro. Mkutano huo ulijadili na kupitia mpango kazi wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mhandisi Saidy alisema kuwa kwa sasa wakala huo unatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 7,500, na kazi hiyo inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.
Aliongeza kuwa pamoja na kazi inayoendelea katika vitongoji hivyo, REA inatarajia kuanzisha mradi mwingine mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 9,000 nchini.
“Kwa sasa kazi inaendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji 7,500 ndani ya miaka miwili, na hivi sasa tuna mradi mpya mwingine wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 9,000, na hii itaifanya REA ndani ya miaka mitatu tuwe tumefikisha umeme kwenye vitongoji 16,500,” alisema Mhandisi Saidy.
“Nasema watu wasiichukulie ‘powa’ REA, sisi tunafanya kazi, na hili si jambo dogo. Ninawapongeza wafanyakazi wa Wakala kwa kazi hii,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), hadi sasa Tanzania ina mikoa 26, wilaya 139, halmashauri 184, tarafa 570, kata 3,956, vijiji 12,319, vitongoji 64,384, pamoja na mitaa 4,263.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo alisema kuwa REA ina matarajio makubwa ya kufanikisha miradi hiyo kutokana na mifumo iliyowekwa ya kuwasimamia wakandarasi namna ya kuwajibika baada ya kuingia nao mikataba ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Saidy alisema kuwa ili kuwawezesha wananchi wa vijijini kutumia nishati safi ya kupikia, wakala huo umeanzisha mradi wa ugawaji wa majiko banifu kama njia mojawapo ya kupunguza upotevu wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mhandisi Saidy alisema kuwa mradi huo umefanikiwa kuwafikia wananchi 5,000 wa maeneo mbalimbali ya vijijini, na wengine 300,000 wanatarajiwa kufikiwa na majiko hayo hivi karibuni baada ya wakala kusaini mikataba ya usambazaji wa majiko hayo.
Alisema kuwa mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi wa maeneo ya vijijini ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua nishati ya gesi, huku pia ukilenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.
“Changamoto ya gesi ni kwamba ikiisha itabidi utoe fedha kupata nyingine, lakini tunafahamu hali za wananchi wetu kulipa shilingi 22,000 wakati mwingine ni mtihani,” alisema.
“Mtumiaji wa gesi hatashawishika kununua nyingine wakati akitoka ndani ya nyumba yake anakutana na msitu, hapo ndio mwanzo wa kukata miti ili apate kuni za kupikia,” alieleza Mhandisi Saidy.
Mhandisi Saidy aliongeza kuwa majiko hayo banifu yametengenezwa kitaalamu na yamepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Yanatarajiwa kutumia kiwango kidogo cha mkaa unaozalishwa na malighafi nyingine mbadala kama pumba.
“Majiko haya banifu ni tofauti na majiko ya mafiga matatu ambayo hutumia kuni na hutoa moshi mwingi, na kusababisha athari za kiafya kwa watumiaji,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Taifa, Dkt. Elias Mtungilwa, alisema kuwa chama hicho kina wajibu wa kusimamia na kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi.