Dunia imepigwa na butwaa kufuatia hukumu nzito iliyotolewa na mahakama nchini Ufilipino dhidi ya Alice Guo, mwanamke wa Kichina aliyefanikiwa kupenya kwenye mfumo wa siasa na kuwa Meya wa mji wa Bamban, huku akiendesha mtandao mpana wa uhalifu. Katika kile kinachoweza kufananishwa na filamu za James Bond, mwanamama huyu mwenye umri wa miaka 36, ambaye jina lake halisi ni Guo Hua Ping, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu, utakatishaji fedha, na uendeshaji wa biashara haramu za kamari.
Hukumu hii iliyotolewa tarehe 20, si tu imemuangukia Guo pekee, bali pia washirika wake saba waliokuwa wakimsaidia katika "dola" yake ya uhalifu, nao wamepigwa nyundo ya kifungo cha maisha.
Dola ya Uhalifu yenye Thamani ya Mabilioni
Mahakama haikuishia kwenye vifungo tu; imeamuru kutaifishwa kwa mali zote zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni ya kamari ya Kichina iliyokuwa chini ya Guo. Mali hizi zinajumuisha eneo kubwa la ardhi lenye ukubwa wa mita za mraba 80,000. Thamani ya mali hizi ni Pesos Bilioni 6, ambayo ni sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 283 (TZS 283 Billion). Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa sana, kinachokaribia bajeti ya maendeleo ya baadhi ya wizara hapa nchini Tanzania, kuonyesha ukubwa wa mtandao huu wa kihalifu.
Aidha, mahakama imeamuru walipwe fidia waathiriwa wote wa biashara hiyo ya usafirishaji haramu wa binadamu, uamuzi ambao umepokelewa kwa mikono miwili na watetezi wa haki za binadamu ulimwenguni.
Mtego Ulinasaje?
Siri ya mtandao huu ilifichuka mwezi Machi mwaka jana, baada ya raia mmoja wa Vietnam kutoroka kutoka kwenye jengo la kifahari lililokuwa likitumika kama ngome ya uhalifu na kutoa taarifa polisi. Jengo hilo, lililokuwa nyuma ya ofisi ya Meya, lilikuwa na kila aina ya anasa—kuanzia mabwawa ya kuogelea hadi majengo ya ofisi—lakini ndani yake kulikuwa na giza nene.
Polisi walipofanya uvamizi wa ghafla, walikuta zaidi ya watu 700 wakiwa wameshikiliwa mateka na kulazimishwa kufanya kazi za utapeli mtandaoni (Online Scams), ikiwemo "Romance Scams" ambazo pia zimeanza kushika kasi katika maeneo mengi Afrika Mashariki. Jambo la kusikitisha na la kushangaza ni kwamba, miongoni mwa waliookolewa walikuwemo raia kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda, Indonesia, Malaysia, Taiwan, na China. Hii inaonyesha kuwa mtandao huu uliokuwa ukiongozwa na "Meya" huyu ulikuwa na makucha yaliyoenea hadi Afrika Mashariki.
Hadithi ya Uongo ya "Mtoto wa Mkulima"
Kwa muda mrefu, Alice Guo alijenga taswira kwa wapiga kura wake kuwa yeye ni mzawa halisi, akidai kuzaliwa na baba Mchina na mama Mfilipino, na kukulia katika mazingira ya kimaskini kwenye mashamba ya nguruwe. Simulizi hii ilimsaidia kushinda kiti cha Umeya wa mji wa Bamban mwaka 2022.
Hata hivyo, methali ya wahenga isemayo "Njia ya mwongo ni fupi" ilitimia. Uchunguzi wa kina uliofanywa na Maseneta wa Ufilipino kwa kushirikiana na Idara ya Upelelezi (NBI) uligundua kuwa alama zake za vidole zililingana na za Guo Hua Ping, raia wa China aliyeingia Ufilipino mwaka 2003. Hii ilithibitisha kuwa alikuwa "pandikizi" aliyepachikwa kwa maslahi ya kijasusi na kibiashara.
Baada ya kuvuliwa madaraka na uraia wake wa Ufilipino kufutwa, Guo alitoroka nchi na kuanza maisha ya ukimbizi akizunguka nchi za Malaysia, Singapore na Indonesia. "Mkono wa sheria ni mrefu," kwani hatimaye alikamatwa jijini Jakarta, Indonesia mwezi Septemba na kurejeshwa Ufilipino kujibu mashtaka.
Sakata hili limetokea wakati kukiwa na mvutano mkali wa kidiplomasia kati ya Ufilipino na China kugombea umiliki wa maeneo katika Bahari ya Kusini ya China, huku Ubalozi wa China ukikaa kimya juu ya kadhia hii. Hukumu hii inatoa funzo kubwa kwa mataifa mengine, ikiwemo Tanzania, juu ya umuhimu wa uhakiki wa kina kwa viongozi na wawekezaji wa kigeni ili kulinda usalama wa taifa.