Wakati taifa la Nepal likijaribu kuinuka kutoka kwenye majivu ya ghasia na maandamano ya umwagaji damu yaliyoangusha serikali, jina moja lisilo la kawaida limeibuka na kuwa gumzo kama kiongozi ajaye: Balendra Shah, msanii wa zamani wa muziki wa Rap mwenye umri wa miaka 35, ambaye sasa ni Meya wa mji mkuu, Kathmandu.
Kuinuka kwa Shah kunakuja baada ya maandamano makubwa yaliyoongozwa na vijana kupinga hatua ya serikali kufungia mitandao 26 ya kijamii na rushwa iliyokithiri. Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 22, mamia kujeruhiwa, na Waziri Mkuu Khadga Prasad Sharma Oli kulazimika kujiuzulu.
Sasa, kundi la vijana la ‘Gen Z Nepal’ lililoongoza mapinduzi hayo, limempendekeza rasmi Meya Shah kuwa mwakilishi wao katika serikali ya mpito itakayoundwa. Kitendo hiki kimemweka katika nafasi ya juu ya kuwa Waziri Mkuu ajaye, huku akipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa vijana wanaotamani mabadiliko.
Katika mitandao ya kijamii kama X (zamani Twitter), vijana wanamiminika kumuunga mkono. "Wewe unapaswa kuwa Waziri Mkuu wetu mpya. Nepal isonge mbele!" aliandika kijana mmoja. Mwingine aliongeza, "Tunataka ufanye kazi na viongozi wengine wasio na rushwa ambao wameonesha uwezo, uadilifu na upendo kwa nchi."
Katika siasa za kihafidhina za Nepal, Shah ni mhusika wa kipekee. Alipata umaarufu kama msanii wa Rap aliyetumia mashairi makali kuikosoa serikali kwa rushwa na uzembe. Wimbo wake maarufu, ‘Balidan’ (Sadaka), wenye watazamaji zaidi ya milioni 11 kwenye YouTube, una mashairi kama: "Wote walioahidi kulinda nchi wameshindwa, wanasiasa wote ni wezi, wanaipora nchi... Hii ni biashara, sio siasa... Siogopi kusema ukweli, je, ni kinyume cha sheria kupaza sauti?"
Mwaka 2022, alitikisa mfumo wa siasa wa nchi hiyo aliposhinda umeya wa Kathmandu kama mgombea huru, akiwashinda wagombea wa vyama vikongwe. Akiwa meya, ameendeleza mtindo wake wa uasi, mara nyingi akivaa koti jeusi na miwani ya jua. Amechukua hatua za dhati dhidi ya rushwa, ikiwemo kuzibana shule binafsi zilizokuwa zikikwepa kodi, na ameboresha miundombinu ya jiji kwa watembea kwa miguu.
Wakati Nepal ikitafuta njia mpya, Balendra Shah, akiwa na uungwaji mkono wa umma na historia ya kupinga mfumo, anaonekana kuwa ishara ya matumaini kwa kizazi kinachodai mabadiliko ya kweli.